Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Neymar amekiri kuzozana na mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Luis Campos lakini ameshangaa na kuhoji aliyevujisha habari hiyo kwenye vyombo vya habari.
Inadaiwa tukio hilo lilitokea Jumamosi baada ya PSG kufungwa mabao 3-1 na Monaco ndipo Neymar akiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo alimalizia hasira zake kwa wachezaji wenzake na Campos.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mechi yao ya leo Jumanne ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern, Neymar alisema mizozano kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ni sehemu ya soka.
“Ni mambo yanayotokea, mjadala mdogo, kuna jambo hatukukubaliana, ni sehemu ya soka, ni mambo yanayotokea kila siku lakini nawapenda wote,” alisema Neymar katika mkutano huo jana Jumatatu.
“Ni kama ilivyo na rafiki yangu wa kike, soka si tu mambo ya urafiki na mapenzi, kuna kuheshimiana pia lakini inatokea kunakuwa na kutoelewana na mijadala wakati mwingine inahitajika ili kusaidia kuweka mambo sawa,” alisema Neymar.
“Hatujazowea kushindwa, kwa hiyo ni dhahiri kwamba tunapopoteza mechi hilo linatusumbua lakini ni njia mojawapo ya kuweka mambo sawa,” aliongeza.
Neymar ambaye pia ni mchezaji wa kimataifa wa Brazil alisema kwamba amekerwa kwa namna ambavyo uvumi umeendelea kujitokeza kumhusu yeye na maisha yake ya soka akiwa PSG.
“Kuna wakati kuna uvumi unatoka kwenye vyombo vya habari, uvumi wenye nia ovu, unazunguka duniani kote kwa haraka, wengi wanasikia uvumi huo na kuna wakati huwa ni uwongo, inachanganya,” alisema.
“Huu ni msimu wangu wa sita PSG, tangu nije hapa imekuwa ikitokea uvumi unakuja wakati wa tukio muhimu la kwenye msimu, wakati wote mimi nakuwa kwenye uvumi huo,” alisema akionekana kushangaa.
“Sina la kufanya kuhusu hilo, sihusiki, mimi ni mchezaji katika klabu lakini uvumi unawakera makocha na wachezaji wenzangu, kwa hiyo ni lazima tujiulize nini kinaendelea kwa sababu haiwezekani kila kitu kinachotokea ndani kinaishia kwenye vyombo vya habari,” alisema Neymar akilalamika.
“Inasikitisha kwa sababu kuna mambo yanatakiwa yawe baina yetu sisi, lazima tuhakikishe hayatoki nje ya vyumba vya kubadilishia nguo na kuwafikia marafiki na wanafamilia,” alitahadharisha.
