Liverpool, England
Ushindi wa mabao 2-0 ambao Liverpool imeupata mbele ya mahasimu wao, Everton umemfariji kocha wa timu hiyo, Jurgen Klopp ambaye amekuwa akipata matokeo mabaya kwa muda mrefu sasa.
Ushindi huo uliotokana na mabao ya Mohamed Salah dakika ya 36 na nyota mpya wa timu hiyo Cody Gakpo dakika ya 49, ambaye hilo ni bao lake la kwanza tangu kujiunga na timu hiyo Januari mwaka huu.
Mbali na imani kwamba bao hilo litampa Gakpo ari ya kuendelea kutupia, Klopp ushindi huo unampa hisia za Liverpool yenyewe na anapata picha ya mfanano wa Liverpool yenyewe.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo tangu kuanza mwaka 2023 na hivyo huenda ukapunguza hofu iliyoibuka ya kutimuliwa kwa Klopp licha ya mwenyewe kusisitiza kwamba haondoki na bado yupo.
Kwa upande mwingine matokeo hayo ni pigo la kwanza kwa kocha mkuu mpya wa Everton, Sean Dyche ambaye alikianza kibarua hicho na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya vinara wa EPL, Arsenal wiki iliyopita.
Akizungumzia ushindi huo, Klopp alisema, “ushindi huu ni faraja kubwa, unapocheza vizuri ndipo unapokuwa katika nafasi nzuri ya kushinda, kiwango cha uchezaji kwa ujumla kilikuwa muhimu kwetu kwa sababu tulihitaji kuwa na la kusema.”
Katika siku za karibuni mwenendo wa timu hiyo umekuwa wa hovyo, vipigo vya hivi karibuni dhidi ya Brentford, Brighton na Wolverhampton vilitosha kuibua mjadala kuhusu hatma ya Klopp katika timu hiyo.
Klopp mwenyewe aliwahi kukiri kwamba vipigo hivyo viliwaweka katika wakati mgumu lakini anaamini baada ya changamoto hiyo, hatimaye ushindi dhidi ya Everton utakuwa umeamsha ari katika timu.
Kimataifa Ushindi wamfariji Klopp
Ushindi wamfariji Klopp
Read also
