Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza amesema ana imani timu yake itaanza vizuri mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kushinda kesho dhidi ya Horoya AC ya Guinea.
Ntibazonkiza hakujumuishwa kwenye orodha ya wachezaji waliosafiri kwenda Conakry, Guinea kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi kutokana na kuumia kifundo cha mguu kwenye mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Singida Big Stars.
Kiungo huyo aliyepo kwenye kiwango bora hivi sasa ameeleza kuwa imani yake inatokana na maandalizi waliyoyafanya na rekodi iliyokuwa nayo timu hiyo kwenye mashindano ya kimataifa.
“Nina imani kubwa na timu yangu pamoja na kikosi kilichokwenda Guinea, kila mchezaji ana njaa ya kutaka kuonekana kupitia mashindano haya lakini rekodi ya Simba kwenye mashindano haya ni ya kipekee kwa Tanzania ndio maana naamini tutashinda,” alisema Ntibazonkiza.
Mchezaji huyo alisema anajua kuwa Horoya si timu ya kubeza na ina rekodi nzuri kama Simba lakini bado nafasi ya ushindi anaipa timu yake kutokana na mikakati waliyojiwekea kwenye michuano hiyo.
Alisema ukitoa wachezaji kitu kingine kinachomvutia ni mbinu za benchi lao la ufundi chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na msaidizi wake namba moja Juma Mgunda ambao wamekuwa bora kwenye kuusoma mchezo na kubaini mbinu mbadala za kuwapa ushindi.
Ntibazonkiza anatarajiwa kuwepo katika mchezo ujao dhidi ya Raja Casablanca ambao utachezwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
