Na mwandishi wetu
Kocha wa Ihefu FC, Zuber Katwila amesema siri ya ushindi wanaoendelea kuupata kwenye Ligi Kuu NBC ni muunganiko waliokuwa nao wachezaji wao pamoja na usajili walioufanya kwenye dirisha dogo.
Ihefu ambayo msimu huu iliweka rekodi ya kutibua rekodi ya Yanga ya kutofungwa michezo 49, juzi iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, matokeo ambayo yaliwapandisha hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.
Akizungumza na GreenSports, kocha huyo ameeleza kuwa kiwango kinachooneshwa na timu yake walikitarajia tangu mwanzo wa msimu na hiyo ilitokana na usajili mzuri walioufanya msimu huu ikiwemo nyota wenye uzoefu mkubwa na ligi ingawa mambo hayakwenda sawa kwenye mechi zao za awali.
“Ukweli matokeo tunayopata hatubahatishi yanatokana na ubora wa wachezaji tuliokuwa nao ingawa hiki kinachotokea kimechelewa na mashabiki ni mashahidi tulikuwa tunacheza vizuri lakini hatupati ushindi lakini kwa sasa tunapata vyote, hii ndio faida ya uvumilivu,” alisema Katwila.
Kocha huyo alisema kuwa anaamini wimbi hilo la ushindi litaendelea katika mechi nane zilizobaki, lengo lao likiwa ni kumaliza msimu kwenye nafasi za juu zaidi ya walipo hivi sasa.
Ihefu ikiwa katika nafasi ya saba, imekusanya pointi 26 baada ya ushindi wa mechi nane, sare mbili na kufungwa mara 12.
