Istanbul, Uturuki
Winga wa kimataifa wa Ghana anayechezea Hatayaspor ya Uturuki, Christian Atsu ni kati ya watu waliopatikana wakiwa majeruhi baada ya tetemeko la ardhi kutokea jana Jumatatu katika nchi za Uturuki na Syria.
Atsu (31) aliyewahi pia kuzichezea Chelsea na Newcastle, Jumapili alikuwa uwanjani na kufunga bao pekee na la ushindi wakati timu yake ya Hataysor ikitoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kasimpasia.
Saa kadhaa baada ya mechi hiyo iliyochezwa usiku, mchezaji huyo hakujulikana alipo huku kadhia ya tetemeko hilo ikiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiathiri miji kadhaa nchini Syria na Uturuki.
Awali msemaji wa klabu ya Hatayspor, Mustafa Ozat aliviambia vyombo vya habari kwamba Christian Atsu pamoja na mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Taner Savut hawajulikani walipo.
Ozat pia alisema kwamba tayari wachezaji wengine wawili wa klabu hiyo wameokolewa na klabu hiyo ilikuwa ikiendelea na jitihada za kuwaokoa wengine ingawa Atsu na Savut ndio bado hawajapatikana.
Kupatikana kwa mchezaji huyo akiwa majeruhi kumetuliza hali ya hofu iliyotanda ingawa haijaweza kujulikana ukubwa wa majeraha aliyoyapata mchezaji huyo ambaye nyumba ya ghorofa aliyokuwa akiishi iliathiriwa na tetemeko hilo.
Tetemeko hilo linadaiwa kusababisha vifo vya watu wapatao 4,000 katika nchi za Uturuki na Syria huku wengine mamia wakiwa majeruhi na wengine wakiachwa bila makazi.
Tetemeko hilo lilitokea mara mbili, la kwanza likipiga saa 10 alfajiri na la pili mchana huku la lile la pili likidaiwa kuwa kubwa zaidi likitajwa kwa kipimo cha 7.7 (magnitude 7.7).
Kimataifa Tetemeko lapiga Uturuki, mchezaji ajeruhiwa, aokolewa
Tetemeko lapiga Uturuki, mchezaji ajeruhiwa, aokolewa
Read also