London, England
Wakati klabu ya Arsenal ikiendelea na msimamo wake wa kutaka kumsajili Moises Caicedo, klabu ya Brighton nayo imeendelea kukomaa ikisisitiza kuwa kiungo huyo hauzwi.
Hii ni mara ya pili kwa Arsenal kuwasilisha rasmi maombi ya kutaka kumnunua mchezaji huyo wa kimataifa wa Ecuador ikidaiwa kuwa tayari kutoa kitita cha Pauni 70 milioni huku Chelsea iliyokuwa ikichuana na Arsenal ikionekana kukata tamaa.
Wiki iliyopita, Arsenal na Chelsea ziliwasilisha ofa tofauti za kumtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 na zote zilikataliwa lakini Arsenal hawajakata tamaa wakiamini Brighton watakuwa tayari kufanya biashara.
Caicedo mwenyewe aliwaarifu mabosi wa Brighton kwa maandishi akidai anataka kuondoka lakini klabu hiyo ilimjibu kwamba hauzwi na kumtaka apumzike hadi baada ya siku ya mwisho ya dirisha la usajili ambayo ni kesho Jumanne.
Jana Jumapili Caicedo aliikosa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Liverpool, mechi ambayo timu yake ilipata ushindi wa mabao 2-1 huku kocha wa Brighton, Roberto de Zerbi akisema anataka mchezaji huyo amalize msimu akiwa na timu hiyo.
Brighton inashika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu England (EPL) ikiwa nyuma ya Tottenham kwa tofauti ya pointi tano lakini Tottenham imecheza mechi 21 hadi sasa na Brighton imecheza mechi 19.
“Mwenyekiti (wa Brighton), Tony Bloom anajua vizuri maoni yangu, tulimpoteza Trossard, tukimpoteza tena na Caicedo itakuwa tatizo kwetu kama tuna nia ya kupambania nafasi Ulaya, kama hatutampoteza Caicedo tutakuwa tayari kupambana,” alisema De Zerbi.
Brighton ambao walimuuza Trossard Arsenal kwa ada ya Pauni 21 milioni mapema mwezi huu, inadaiwa wamekataa ofa ya kwanza ya klabu hiyo ya Pauni 60 milioni kwa Caicedo pamoja na ofa ya Chelsea ya Pauni 55 milioni.
Hadi sasa Caicedo ameichezea Brighton mechi 26 za EPL na kufunga mabao mawili na ana mkataba unaofikia ukomo mwaka 2025 huku ikidaiwa kwamba mabosi wake wamechukizwa na kauli ya mchezaji huyo kutaka kuondoka na ndio maana wakampa ‘likizo fupi’ isiyo rasmi.
Kimataifa Brighton yaikomalia Arsenal, Caicedo hauzwi
Brighton yaikomalia Arsenal, Caicedo hauzwi
Related posts
Read also
