Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo ameeleza kuwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Azam kilisababishwa na kukosekana ubora kwa wachezaji wake.
Prisons ilikubali kipigo hicho cha pili mfululizo kwenye ligi katika mchezo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Odhiambo alisema kwamba kimbinu walijipanga sawasawa na walikuwa bora katika hilo lakini kukosekana ubora wa mchezaji mmoja mmoja ndiko kulikowagharimu na kupoteza mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao.
“Tumepoteza kwa sababu hatukuwa na ubora unaotakiwa, kama ukiangalia bao la kwanza hatukuwa makini kutoka katikati ya uwanja mpaka wanakwenda kufunga bao wapinzani, ni kama ilivyokuwa bao la tatu pia ni ubora tu wa mchezaji mmoja mmoja ulitugharimu.
“Si nzuri kuendelea kupoteza mechi kwa mabao mengi kama hivi, tutakwenda kufanya marekebisho kidogo pia kwenye ulinzi, maana safu ya ulinzi imekuwa ikiwapa sana mianya wapinzani kuliona goli letu mara kwa mara,” alisema Odhiambo.
Kwa upande wa Azam, kocha msaidizi wa timu hiyo, Aggrey Morris alisema wanashukuru kuona kila kitu kilikuwa kama walivyopanga, kujituma kwa wachezaji, kupambana kwao ndiyo kumewapa matokeo, hivyo anawapongeza wachezaji wake.
“Nachoweza kusema hali ya mchezo ilikuwa nzuri kwa pande zote ukiangalia mechi ilivyokuwa, nawapongeza Prisons wamejitoa na kupambana lakini timu yangu pia imejituma, imefuata maelekezo na tumepata matokeo kwa hiyo tunashukuru Mungu kwa hilo,” alisema Morris.
Soka Kocha Prisons alia na ubora
Kocha Prisons alia na ubora
Related posts
Read also
