Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga inatarajia kurejea mazoezini keshokutwa Alhamisi kuanza maandalizi ya michuano iliyo mbele yao baada ya kupumzika kwa siku tano tangu iliporejea kutoka Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi.
Yanga ilirejea Dar es Salaam Jumamosi iliyopita baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kwa mujibu wa ratiba ya benchi la ufundi wachezaji ambao hawakushiriki Kombe la Mapinduzi watarejea kambini keshokutwa wakati walioshiriki wanatarajiwa kurejea Ijumaa hii.
“Baada ya Mapinduzi, timu sasa inarejea kuanza kambi ya kujiandaa na mechi za ligi lakini pia kuanza maandalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na ile ya Kombe la Azam Sports (Kombe la FA),” alisema Kamwe.
Ofisa huyo alifafanua kuwa kambi hiyo pia itajumuisha wachezaji waliokwenda mapumziko wakiwa na majeraha akiwemo kipa Abuutwalib Msheri na mshambuliaji Denis Nkane ambao watafanyiwa vipimo mazoezini kujua maendeleo yao.
Yanga inatarajia kurejea dimbani Januari 16, mwaka huu kuvaana na Ihefu kwenye mechi ya Ligi Kuu NBC itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Timu hiyo pia inatarajia kuanza kampeni yake ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi Februari 12 dhidi ya US Monastir ya Tunisia kabla ya Februari 19 kuvaana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kufuatiwa na mechi dhidi ya Real Bamako ya Mali Februari 26, mwaka huu.
Soka Yanga kuanza mazoezi Alhamisi
Yanga kuanza mazoezi Alhamisi
Related posts
Read also