Los Angeles, Marekani
Nahodha wa timu ya Taifa ya Wales, Gareth Bale ametangaza rasmi kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 33 akiacha rekodi ya kucheza mechi nyingi na kuifungia mabao mengi timu yake ya Taifa.
Bale anastaafu akiwa ameifungia timu hiyo mabao 44 na kucheza mechi 111 akiwa pia na rekodi ya kubeba mara tano taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na lile la La Liga mara tatu akiwa na Real Madrid, alitangaza uamuzi huo kupitia mitandao ya kijamii.
“Baada ya kutafakari kwa umakini mkubwa, natangaza kustaafu kucheza soka la kimataifa pamoja na kwenye klabu, najiona mwenye bahati kwa kutimiza ndoto yangu ya kucheza mchezo nilioupenda,” alisema Bale katika taarifa hiyo.
Bale, mzaliwa wa Cardiff alianza kupata umaarufu katika klabu ya Southampton kabla ya kujiunga na Tottenham Hotspur na hatimaye mwaka 2013 alisaini mkataba ulioweka rekodi ya dunia alipojiunga na Real Madrid kwa ada ya Pauni 80 milioni kabla ya kuhamia Marekani Juni mwaka jana na kujiunga na klabu ya Los Angeles FC (LAFC).
Mchezaji huyo ndiye aliyeiongoza vyema Wales hadi kukata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kufuzu fainali hizo tangu mwaka 1958.
Rekodi ya kubeba mataji matano ya Ligi ya Maabingwa Ulaya inamfanya awe mchezaji pekee wa Uingereza mwenye rekodi hiyo pamoja na ile ya kubeba mataji matatu ya Kombe la Dunia la Klabu akiwa pia na Real Madrid.
“Ni soka ndilo lililonipa mambo ya kipekee katika maisha, nimekuwa juu katika misimu 17, hilo ni jambo kubwa bila kujali nini kinaweza kufuata katika maisha yangu mengine,” alisema. Bale
Mwaka 2019, Bale alitaka kuhamia China kucheza soka katika klabu ya Jiangsu Suning lakini inadaiwa kwamba mpango huo ulizimwa na mabosi wa Real Madrid.
Alirudi Tottenham kwa mkopo msimu wa 2021/22 na kufunga mabao 17 kabla ya kurudi Real Madrid na kucheza mechi saba katika msimu uliofuata hizo zikiwa mechi zake za mwisho na klabu hiyo ya nchini Hispania.
Baada ya mkataba wake na Real Madrid kufikia ukomo, Bale alitimkia nchini Maarekani na kujiunga na
LAFC kwa mkataba wa mwaka mmoja ingawa mambo hayakuwa mazuri kutokana na kuandamwa na janga la majeraha ya mara kwa mara, alicheza mechi 13 tu, mbili akianza kipindi cha kwanza lakini aliisaidia timu hiyo kubeba taji Novemba mwaka jana.
“Najiona nina deni kwa watu wengi kwa kunisaidia kuyabadili maisha yangu na kuniongoza katika maisha ya soka katika namna ambayo ilikuwa kwenye ndoto nilizoziota kwa mara ya kwanza nikiwa na miaka tisa,” alisema Bale.
“Shukran kwa klabu zangu za zamani Southampton, Tottenham, Real Madrid na LAFC, shukran kwa makocha wangu wote wa zamani, wasaidizi, wachezaji wenzangu na mashabiki waliokuwa wakijitoa, mawakala wangu, marafiki zangu wa kipekee na familia, ukubwa wa mchango wenu hauna hesabu.
“Wazazi wangu, dada yangu, bila kujitoa kwenu katika siku za mwanzo, bila msingi huo imara, leo nisingeweza kuandika taarifa hii, kwa hiyo asanteni kwa kuniweka katika njia na kwa ushirikiano wenu usiochoka.
“Mke wangu na watoto wangu, mapenzi yenu na ushirikiano vimenibeba hadi hapa nilipofika, mmekuwa pamoja nami nilipokuwa juu na niliposhuka, mlinihamasisha kuwa bora na kuwafanya muwe na cha kujivunia.”
“Kwa hiyo nasonga mbele nikiwa na matarajio katika hatua nyingine ya maisha yangu, ni wakati wa mabadiliko na kipindi cha mpito na fursa ya mambo mengine mapya.”
Bale inaaminika kwamba amelazimika kuchukua uamuzi wa kustaafu soka kutokana na kuandamwa mara kwa mara na majeraha ambayo yamekuwa yakimnyima kuonyesha ubora wake uliozoeleka kwenye soka.
