Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amekiri ana kazi ya kufanya kurekebisha kikosi chake kuelekea mechi zinazofuata baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar jana lakini amewapongeza vijana wake kwa kazi kubwa waliyofanya na kukiri mechi ilikuwa ngumu.
Simba ilipata sare hiyo kwenye mechi ngumu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ambapo Kagera ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Deus Bukenya kabla ya Henock Inonga kuchomoa bao hilo.
Mgunda ameeleza kuwa mechi hiyo imekuwa ngumu kama alivyotarajia kulingana na aina ya wapinzani waliokutana nao lakini anashukuru kuvuna alama moja ingawa imewapunguzia kasi kwenye mbio zao za ubingwa lakini watarekebisha makosa kuhakikisha wanakaa sawa.
“Tunashukuru Mungu mpira umeisha salama tumepata alama moja, ni mechi ambayo tangu mwanzo nilifahamu itakuwa ngumu kutokana na mtindo wa soka la wapinzani lakini pia kulikosekana umakini wa kukaba tukafungwa lakini mwisho tukasawazisha.
“Lakini yote kwa yote kuna kitu tumekipata, nimekiona kama mwalimu kwamba tunakwenda kuviongezea ili tufanye vizuri kwenye mechi zijazo, japo kikubwa nawapongeza vijana wangu wamefanya kazi kubwa siyo rahisi hii mechi ilikuwa ngumu na kila mmoja analijua hilo, tutakwenda kujipanga zaidi,” alisema Mgunda.
Upande wake kocha wa Kagera, Mecky Maxime amesema sare hiyo ni kama ushindi kwao kutokana na mechi ngumu ya mwisho aliyotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam, hivyo kupata sare nyingine dhidi ya Simba ni ushindi tosha kwao.
“Kwanza hizi mechi mbili kwangu mimi nimeshinda kutokana na timu nilizocheza nazo, timu ina kocha mkubwa, wachezaji wakubwa, yaani kwangu sina la kujilaumu kwa vijana nawapongeza. Kuna muda unakuwa mkweli kama kuna watu wamekuzidi na unaingia kwa tahadhari na unawamudu, ni kitu kizuri kwa hiyo nawapongeza sana vijana wangu wamefanya kazi nzuri.” alisema Maxime
“Na nampongeza Mgunda, timu iko vizuri najua wao watakuwa wamepoteza kwa sababu timu ipo kwenye mbio za ubingwa lakini mchezo ulikuwa mzuri kwa kweli,” alisema Maxime.
Kwa matokeo hayo, Simba imeendelea kusalia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu NBC ikiwa na pointi 38, pointi sita nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 44 baada ya wote kucheza mechi 17 huku Kagera ikiwa nafasi ya sita kwa pointi 23.
