Sao Paulo, Brazil
Mwanasoka gwiji wa Brazil, Pele hali yake inaelezwa kuzidi kuwa mbaya kutokana na maradhi ya saratani (kansa) yanayomsumbua kuongezeka.
Septemba mwaka jana Pele aliondolewa uvimbe ili kukabiliana na maradhi ya saratani na tangu wakati huo amekuwa akipata tiba ya maradhi hayo kila mwezi lakini habari za ndani kutoka hospitali ambayo anatibiwa zilizopatikana jana zilieleza kuwa hali ya mwanasoka huyo aliyetwaa Kombe la Dunia mara tatu inazidi kuwa mbaya na anahitaji uangalizi wa karibu.
Mtoto wa kike wa Pele, Kely Nascimento katika kauli yake aliyoitoa kupitia mitandao ya kijamii alisema kwamba baba yake huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 82 anatarajia kula Sikukuu ya Krismasi akiwa hospitali ya Albert Einstein.
“Sherehe za Krismasi kwa upande wetu hazitakuwapo nyumbani, tumeamua na madktari kwamba kwa sababu mbalimbali itakuwa vizuri kwetu kuendelea kuwa hapa na kupata huduma zote ambazo zinapatikana hapa hospitali,” alisema Kely kupitia mtandao wa Instagram.
Mara baada ya kufikishwa hospitali hivi karibuni, Pele alinukuliwa mwenyewe akisema kwamba matibabu yanakwenda vizuri hasa katika mfumo wa upumuaji na kwamba alikuwa akiendelea kupata tiba ya maradhi ya saratani kama kawaida ingawa habari za jana zinakuwa mpya na zimeibua hali ya wasiwasi kuhusu afya ya gwiji huyo wa soka duniani.
Katika maisha yake ya soka la ushindani, Pele ameweka rekodi ya kuifungia timu ya Taifa ya Brazil jumla ya mabao 77 katika mechi 92 na kuiwezesha kubeba Kombe la Dunia mara tatu kuanzia mwaka 1958, 1962 na 1970.
