Paris, Ufaransa
Mshambuliaji, Karim Benzema ametoa kauli inayoashiria kuachana na timu yaTaifa ya Ufaransa akidai maisha yake ya soka katika timu hiyo yanafikia mwisho.
Benzema ambaye janga la kuwa majeruhi lilimnyima nafasi ya kuiwakilisha Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia za Qatar zilizomalizika Jumapili hii na Argentina kuibuka bingwa, ametumia mtandao wa Twitter kutoa kauli hiyo akifafanua kwamba safari yake inafikia ukomo.
Mshambuliaji huyo ambaye pia anaichezea klabu ya Real Madrid ya Hispania jana Jumatatu alifikisha umri wa miaka 35, alianza kuichezea timu ya Ufaransa kwa mara ya kwanza Agosti 2007 katika mechi dhidi ya Austria.
Nimeandika historia yangu, na nilifanya makosa hadi kufika hapa nilipo leo, na najivunia hilo,
alisema kupitia mtandao huo akiwa anajivunia kuichezea Ufaransa mara 97 na kufunga mabao 37 na kwa alichosema ni wazi kwamba anastaafu kuichezea timu hiyo.



Ufaransa ilitarajia kumtumia Benzema ili kulitetea Kombe la Dunia lakini akaumia na hivyo kuondoka katika kikosi ambacho hatimaye kilipambana hadi kufikia hatua ya fainali kabla ya kulala kwa mikwaju ya penalti 4-2 kwa Argentina waliotawazwa mabingwa wapya wa dunia.
Benzema amekuwa na bahati mbaya na timu ya Ufaransa, alikosekana kwa takriban miaka sita baada ya kuingia katika kashfa na mchezaji mwenzake Mathieu Valbuena iliyohusisha mabinti wa umri chini ya miaka 18 kabla ya kurudi na kuiwakilisha kwenye Euro 2020.
Mshambuliaji huyo amekuwa msaada mkubwa katika klabu ya Real Madrid akiiwezesha kutwaa taji la 14 la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita pamoja na yeye mwenyewe kutwaa tuzo yake ya kwanza ya Ballon d’Or.
