Doha, Qatar
Morocco, leo Jumamosi imekuwa timu ya kwanza Afrika kufikia hatua ya nusu fainali katika historia ya Kombe la Dunia baada ya kuitoa Ureno kwa bao 1-0 katika mechi ya robo fainali, matokeo yaliyotosha kumliza nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo.
Baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, Ronaldo alionekana akiingia katika vyumba vya kubadilishia nguo huku akilia wakati mashabiki na wachezaji wa Morocco wakipagawa kwa furaha baada ya kuweka historia mpya ya fainali hizo.
Shujaa wa Morocco alikuwa ni mshambuliaji, Youssef En-Nesyri katika dakika ya 42 akiunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Yahya Attiyat-Allah. En-Nesyri alikwenda juu na kuupiga mpira uliomshinda kipa wa Ureno Diogo Costa.
Bao hilo liliamsha shangwe kwa mashabiki wa Morocco waliojazana kwenye Uwanja wa Al Thumama na kuutawala kwa namna walivyokuwa wakiishangilia timu yao mwanzo mwisho.
Nahodha wa Ureno, Bruno Fernandes nusura asawazishe bao hilo lakini shuti alilopiga liligonga mwamba na kuishia kuibua mshtuko kwa mashabiki wa Morocco.
Dakika tano baada ya mapumziko, kocha wa Ureno, Fernando Santos alimuingiza Ronaldo ambaye hata hivyo hakuweza kubadili matokeo ya mchezo huo licha ya kuisumbua safu ya ulinzi ya Morocco mara kadhaa.
Katika kipindi cha pili, Morocco walitumia muda mwingi kujihami kwa umakini wa hali ya juu na katika dakika za majeruhi, timu hiyo ilipata pigo baada ya mshambuliaji wake, Walid Cheddira kupewa kadi ya pili ya njano kwa kucheza rafu na hivyo kuwa nyekundu lakini upungufu huo wa mchezaji mmoja haukuweza kuisaidia Ureno isawazishe bao hilo.
Morocco pamoja na kutumia muda mwingi kujihami lakini haikuacha kuichachafya Ureno na kama si umakini wa safu ya ulinzi ya timu hiyo shambulizi moja la kushtukiza lingeweza kuiumiza zaidi Ureno iliyokuwa ikihaha kusaka bao la kusawazisha.
Ushindi wa Morocco unakuwa historia mpya ya fainali za Kombe la Dunia kwa Afrika ikiwa timu ya kwanza kufikia hatua ya nusu fainali, hapo kabla timu tatu za Cameroon, Senegal na Ghana zilikuwa zikishikilia rekodi ya kufikia hatua ya robo fainali.
Ushindi wa Morocco pia unakumbusha kauli iliyowahi kutolewa na kocha wa timu hiyo, Walid Regragui ambaye baada ya kufuzu hatua ya mtoano alisema kwamba si vibaya kwa timu hiyo kuota kulibeba Kombe la Dunia.
Baada ya ushindi huo wakati mashabiki wakiimba na kushangulia majukwaani, Regragui alibebwa na kurushwa juu na wachezaji wake na sasa kikosi chake kinasubiri mechi ya nusu fainali na mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali baadaye leo kati ya Ufaransa na England.
Kimataifa Morocco yaweka historia Afrika
Morocco yaweka historia Afrika
Read also
