Doha, Qatar
Mshtuko, ndoto za Brazil kubeba taji la sita la dunia zimezimwa rasmi na Croatia, ulimwengu wa soka umeachwa katika mshtuko mkubwa huku kipa wa Croatia, Dominik Livakovic akiendeleza umahiri wake wa kuokoa mikwaju ya penalti.
Brazil hatimaye jana Ijumaa iliaga rasmi fainali za Kombe la Dunia ikiwa moja ya timu iliyopewa nafasi kubwa ya kulibeba taji hilo lakini ikajikuta ikianguka kwa mikwaju ya penalti mbele ya Croatia baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 120.
Kipa Livakovic hakuwa jina kubwa kama ilivyo timu yake ya Croatia ambayo haikuwa ikitajwa kama ingeweza kufika ilipofika lakini imefika tena kwa kuitoa timu kubwa na sasa inasubiri kucheza hatua ya nusu fainali dhidi ya Argentina ambayo iliitoa Uholanzi kwa penalti 4-3 baada ya sare ya mabao 2-2 katika mechi nyingine ya robo fainali na tayari Croatia imeanza kutajwa kwamba inaweza kufanya maajabu.
Katika kipindi kisichozidi wiki moja, Livakovic ameibeba Croatia mara mbili kwenye penalti, alianza kuonyesha umahiri Jumatatu iliyopita katika hatua ya mtoano dhidi ya Japan kwa kuokoa penalti tatu na jana akaendeleza tena umahiri huo huo kwa kuiwezesha Croatia kuiangusha Brazil akiokoa mkwaju mmoja wa penalti.
Baada ya dakika 120 za mpambano ulioisha kwa sare ya bao 1-1, katika mikwaju ya penalti, Livakovic aliokoa penalti ya kwanza ya Brazil iliyopigwa na Rodrygo. Croatia ilifunga penalti zake nne zilizofuata wakati penalti ya Marquinhos iligonga mwamba na kuzima rasmi ndoto za Brazil huku ikiibua shangwe kwenye benchi la Croatia.
Kocha wa Croatia, Zlatko Dalic alisema kipa wao Livakovic aliokoa penalti ya kwanza jambo ambalo lilikuwa muhimu mno kwao, “Amefanya kile alichotakiwa kufanya, aliokoa penalti ya kwanza iliyotupa hali ya kujiamini na kuwafanya Brazil wakose hali ya kujiamini kwa sababu walianza kuogopa wangepoteza nyingine.”
Kwa kuokoa penalti, Livakovic anaingia katika orodha ya makipa wengine, Sergio Goycochea wa Argentina, Harald Schumacher wa Ujerumani na M-Croatia mwenzake Danijel Subasic ambao wameokoa penalti nne kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia.
Katika mechi hiyo, Livakovic alifungwa bao na Neymar katika dakika chache kabla ya kipindi cha kwanza katika dakika 30 za nyongeza kumalizika lakini Croatia ikasawazisha dakika ya 117 kupitia kwa Bruno Petkovic na hatimaye timu hizo kwenda kwenye mikwaju ya penalti na ndipo Croatia ilipoitumia vizuri nafasi hiyo ikishinda kwa penalti 4-2 kuuachia mshtuko ulimwengu wa soka.
Kimataifa Mshtuko, Croatia yaibwaga Brazil
Mshtuko, Croatia yaibwaga Brazil
Related posts
Read also
