Na mwandishi wetu, Tanga
Simba, leo Jumamosi imenyakua pointi tatu zilizoiwezesha kushika usukani wa Ligi Kuu NBC kwa kufikisha pointi 34 baada ya kuichapa Coastal Union ya Tanga mabao 3-0.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba ilianza kuhesabu mabao yake dakika ya 53 kwa bao lililofungwa na Mosses Phiri kwa mpira ulioanzia kwa Muzamir Yassin aliyempasia Chama ambaye alimpenyezea Phiri naye akampunguza beki mmoja wa Coastal hadi kuanguka chini kabla ya kufumua shuti la chinichini lililojaa wavuni.
Dakika saba baadaye, beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe juhudi zake za kupanda kupeleka mashambulizi zilizaa matunda baada ya kushikwa shati na beki wa Coastal, Lameck Lawi akiwa ndani ya eneo la penalti na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti ambapo Phiri hakufanya makosa kuiandikia Simba bao la pili.
Simba iliandika bao la tatu, safari hii mpira ukianzia kwa Phiri tena ambaye alifumua shuti la juu juu lililookolewa na kipa wa Coastal, Mahmoud na mpira kumkuta John Bocco ambaye aliunganisha kwa kichwa lakini mpira alioupiga uligonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kumkuta Chama ambaye alitulia na kuujaza wavuni kiulaini.
Chama kwa mara nyingine katika mechi ya leo amedhihirisha umuhimu wake ndani ya kikosi cha Simba, baada ya kupata tabu kipindi cha kwanza, kipindi cha pili alikuwa vizuri na kutoa mchango mkubwa kwa timu hiyo hadi kupata ushindi.
Katika mechi ya leo, Coastal nao walionyesha uhai kipindi cha kwanza na kuwadhibiti mara kwa mara wachezaji wa Simba kabla mambo hayajawaharibikia kipindi cha pili na kujikuta wakipoteza pointi kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Coastal katika kipindi hicho cha kwanza, Hamad Majimengi alichezewa rafu na beki wa Simba Joash Onyango na mashabiki wa timu hiyo kutarajia penalti lakini mwamuzi hakuwapa.
Zikiwa zimebakia dakika tano mpira kumalizika, Coastal nusura wapate bao baada ya Majimengi tena kumpiga chenga beki mmoja wa Simba na kumsogelea kipa Beno Kakolanya lakini mpira alioupiga haukuwa na madhara yoyote langoni mwa Simba.
Katika mechi ya leo, Simba ilianza na kipa wake namba moja Aishi Manula ambaye baada ya kipindi cha kwanza alitolewa na nafasi yake kuingia Kakolanya kwa kilichodaiwa kuwa kipa huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo. Simba pia ilipata pigo baada ya Sadio Kanoute kupewa kadi mbili za njano dakika chache kabla ya mpira kumalizika.
Simba sasa wanasubiri matokeo ya mechi ya Yanga na Prisons kesho Jumapili ili kujua kama watakaa kileleni kwa saa 24 au la.
Ushindi wa leo wa Simba pia una maana kubwa kwa Phiri kwani mabao yake mawili yanakoleza moto wa kuwania tuzo ya mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa amefikisha mabao 10 sawa na Fiston Mayele wa Yanga wakifuatiwa na Sixtus Sabilo wa Mbeya City mwenye mabao saba akiwa nafasi ya pili.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo mambo yamezidi kuwa mabaya kwa Ruvu Shooting iliyochapwa Dodoma Jiji mabao 2-1.
Kesho Jumapili, mbali ya mechi ya Yanga na Prisons kwenye Uwanja wa Mkapa, mechi nyingine ya ligi hiyo ni ile ya Geita Gold watakaokuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar.
Soka Simba yainyuka Coastal 3-0
Simba yainyuka Coastal 3-0
Related posts
Read also
