Lusail, Qatar
Cameroon imeweka rekodi ya kibabe ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Brazil katika mechi ya Kundi G ya fainali za Kombe la Dunia licha ya kushindwa kufuzu hatua ya mtoano.
Brazil ambayo ilibadili kwa kiasi kikubwa kikosi chake cha kwanza katika mechi hiyo ikiwa tayari imefuzu hatua ya mtoano, iliadhibiwa kwa bao la Vincent Aboubakar aliyeujaza wavuni mpira kwa kichwa katika dakika za nyongeza (92) akiitumia pasi ya Ngom Mbekeli.
Mfungaji wa bao hilo hata hivyo alijikuta akiadhibiwa kwa kadi ya pili ya njano baada ya kupagawa na bao hilo hadi kujisahau na kushangilia kwa kuvua jezi na mwamuzi kumlima kadi hapo hapo.
Ushindi huo wa kibabe dhidi ya Brazil hata hivyo uliishia kuwa tukio la kujivunia kwani haukuweza kuisaidia timu hiyo kufuzu hatua ya mtoano baada ya Switzerland kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Serbia katika mechi nyingine ya Kundi G, matokeo yaliyotosha kuhitimisha safari ya Cameroon kwenye fainali hizo na kuziacha Brazil na Switzerland zikisonga mbele.
Katika kilichoonekana labda ni kutoipa umuhimu mechi hiyo, kocha wa Brazil, Tite alifanya mabadiliko ya wachezaji 10 huku akimpa nafasi ya Gabriel Martinelli wa Arsenal ambaye aliitumia nafasi hiyo kudhihirisha uwezo wake na mara kadhaa umahiri wa kipa wa Cameroon, Devis Epassy ulikuwa kikwazo kwa Martinelli kuipatia Brazil bao.
Brazil, moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kulibeba taji la Dunia, pamoja na kufungwa na Cameroon imemaliza mechi za makundi ikiwa kinara wa kundi lake na sasa inasubiri kuumana na Korea Kusini katika hatua ya mtoano baada timu hiyo kuifunga Ureno.
Matumaini ya Brazil ambao ni mabingwa wa dunia mara tano, kwa sasa ni kuona nyota wao, Neymar anapona na kuanza kucheza mechi za hatua ya mtoano akiwa fiti baada ya kuumia enka ya mguu wa kulia katika mechi ya kwanza ya Brazil dhidi ya Serbia.
Hatimaye Cameroon au Indomitable Lions (Simba wasiofugika) imeondoka Qatar lakini haikuondoka hivi hivi, imeondoka ikiwa na jambo la kujivunia, imeacha kumbukumbu ambayo mashabiki wake wataendelea kujivunia.
Matokeo mechi za Kombe la Dunia jana Ijumaa…
Kundi G
Cameroon 1-0 Brazil
Serbia 2-3 Switzerland
Kundi H
Ghana 0-2 Uruguay
Korea Kusini 2-1 Ureno
