Doha, Qatar
Raha ya bao la kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia. Ndicho anachojivunia mshambuliaji wa Poland, Robert Lewandowski. Amefunga mabao mengi na timu ya Taifa, ana tuzo nyingi za ufungaji bora lakini hapo kabla hakuwahi kufunga bao kwenye fainali hizo.
Lewandowski mshambuliaji tegemeo wa Barcelona ambaye pia ameifanyia makubwa klabu ya Bayern Munich, kwa sasa amefungua ukurasa mpya jana Jumamosi baada ya kufunga bao wakati Poland ikiibugiza Saudi Arabia mabao 2-0, ushindi ambao umeifanya timu hiyo kushika usukani kwenye Kundi C ambalo pia lina timu za Argentina na Mexico.
Raha ya bao hilo ilikuwa wazi kwa Lewandowski kwa namna alivyofurahia, ni kama vile alikuwa akisubiri kwa muda mrefu kupata bao hilo ambalo lilikuwa la pili kwa timu yake akifunga katika dakika ya 82 kwa kuyatumia makosa ya safu ya ulinzi ya Saudi Arabia.
Bao la kwanza la Poland lilipatikana katika dakika ya 39 mfungaji akiwa ni Piotr Zielinksi ambaye aliitumia vizuri pasi ya Lewandowski.
Saudi Arabia hata hivyo ilionyesha uhai na kupigania ushindi hadi kupata penalti katika kipindi cha kwanza lakini mkwaju wa chinichini wa penalti uliopigwa na Al Dawsari kwanza uliokolewa na kipa na kupigwa shuti la pili na mchezaji mwingine ambalo kipa aliokoa na mpira kuwa kona ambayo haikuweza kuzaa matunda.
Kwa ushindi huo, Poland kwa sasa ndiyo inayoongoza Kundi C ikiwa imekusanya pointi nne ikifuatiwa na Argentina na Saudi Arabia ambazo kila moja ina pointi tatu wakati Mexico inashika mkia ikiwa na pointi moja.
Raha ya Lewandowski hata hivyo itaendelea iwapo ataiwezesha Poland kufuzu hatua ya makundi huku akiendelea kufunga mabao kwani licha ya timu hiyo kushika usukani bado itakuwa na kazi ngumu mbele ya Argentina katika mechi itakayoamua timu ipo inasonga hatua ya mtoano.

Argentina nayo inatambua ugumu wa mechi yake na Poland, baada ya kupoteza mechi na Saudi Arabia iliamua kuja kivingine na kupata ushindi katika mechi yake na Mexico na hivyo kufufua matumaini kama ilivyo kwa Poland.
Saudi Arabia na Mexico ambazo jana zilipoteza mechi zao nazo bado si timu za kubezwa kwani ushindi wa mechi zao za mwisho unaweza kuwa na maana kubwa kwa kutegemea matokeo ya mechi ya Poland na Argentina yatakavyokuwa. Lolote linaweza kutokea.
Matokeo mechi za Jumamosi za Kombe la Dunia…
Kundi C
Poland 2- 0 Saudi Arabia
Argentina 2-0 Mexico
Kundi D
Tunisia 0-1 Australia
Ufaransa 2- 1 Denmark
