Zurich, Uswisi
Fifa imeionya Tunisia kuwa inaweza kuifungia na kuifanya timu ya taifa ya nchi hiyo isishiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar kama serikali ya nchi hiyo haitoacha kuingilia masuala ya soka.
Onyo hilo la Fifa limekuja baada ya kauli zinazojirudia za Waziri wa Vijana na Michezo wa Tunisia, Kamel Deguiche kuhusu uwezekano wa kuuvunja uongozi wa soka nchini humo.
Fifa inaichukulia kauli ya waziri huo kuwa ni mpango wa kuingilia masuala ya uendeshaji wa Shirikisho la Soka Tunisia (FTF) na imetaka shirikisho hilo kutoa ufafanuzi kuhusu mpango wa kuingiliwa kwa utendaji kazi wao pamoja na tishio la kusimamisha utendaj kazi za ofisi za shirikisho hilo.
Katika taarifa yake Fifa imewakumbusha viongozi wa FTF kwamba wanachama wa Fifa wana haki ya kuendesha mambo yao wakiwa huru bila kuingiliwa na mtu yeyote.
“Kutofuata taratibu hizo kunaweza kuwa sababu ya adhabu kwa mujibu wa sheria za Fifa ikiwamo adhabu ya kusimamishwa kwa uanachama wa Fifa wa nchi husika,” ilieleza barua ya Fifa iliyoandikwa na mkurugenzi wa vyama wanachama wa Fifa, Kenny Jean-Marie kwenda kwa katibu mkuu wa FTF, Wajdi Aouadi ambaye anatakiwa hadi Ijumaa awe amejibu barua hiyo.
Iwapo adhabu hiyo itatolewa maana yake ni kwamba Tunisia itasimamishwa kushiriki michuano yote ya soka inayotambuliwa na Fifa zikiwamo fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Novemba 20 mwaka huu ambapo Tunisia imepangwa Kundi D lenye timu za Denmark, Australia pamoja na mabingwa watetezi, Ufaransa na nchi hiyo itatupa karata yake ya kwanza Novemba 22 dhidi ya Denmark.
Kwa kipindi kirefu sasa mabosi wa FTF wamekuwa wakituhumiwa kwa tuhuma kadhaa zikiwamo zile za klabu ya Chebba ambayo imekuwa ikidai kwamba viongozi wa FTF akiwamo rais wake, Wadie Jary waliipotosha Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) kabla ya mahakama hiyo baadaye kutoa hukumu iliyoibeba klabu hiyo.
Mashabiki wa Chebba walichoma moto matairi na kufunga barabara katika mji wao wakipinga adhabu ya kufungiwa waliyopewa na FTF Oktoba 2020, adhabu ambayo baadaye ilifutwa.
Kwa mwaka huu, Fifa tayari imezifungia nchi za Kenya na Zimbabwe kwa sababu ya serikali za nchi hizo kuingilia masuala ya soka. India nayo ilifungiwa na nchi hiyo ilikuwa ifutiwe kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 17 lakini adhabu hiyo ilifutwa na baadaye nchi hiyo kuendelea kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.
Kimataifa Fifa yatishia kuifungia Tunisia
Fifa yatishia kuifungia Tunisia
Related posts
Read also