Bellinzona, Uswisi
Rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter na Rais wa zamani wa Uefa, Michel Platini huenda wakarudishwa mahakamani kwa mara nyingine kujibu tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.
Ofisi ya waendesha mashtaka nchini Uswisi leo imetangaza uamuzi wa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Jinai nchini Uswisi wa kuwaachia huru vigogo wa zamani wa soka baada ya kufutiwa mashitaka hayo Julai mwaka huu licha ya kufanyika uchunguzi dhidi ya washitakiwa hao kwa takriban miaka saba.
Blatter na Platini ambao wamewahi kuwa watu wenye nguvu katika soka duniani, walifikishwa mahakamani ambapo ilidaiwa kuwa Blatter alimlipa Platini malipo yaliyoitwa ya ‘kiungwana’ ya dola 1.99 (zaidi ya Sh 4 bilioni za Kitanzania) kwa kazi ya ushauri aliyokuwa akiifanya kwa Blatter, kazi ambayo ilitiliwa shaka.
Kutokana na kashfa hiyo na nyingine zilizokuwa zikiwakabili, vigogo hao walijikuta wakitimuliwa katika nyadhifa zao Fifa na Uefa lakini Mahakama ya Jinai nchini Uswisi haikuona kosa lolote kwa Blatter kumlipa Platini fedha hizo na kutilia wasiwasi juu ya uhalali wa tuhuma hizo.
Awali baada ya mahakama kuwafutia kesi Blatter na Platini, ofisi hiyo iliahidi ingepitia hukumu hiyo kabla ya kuamua kukata au kutokata rufaa lakini taarifa rasmi ya ofisi hiyo iliyopatikana leo ilidai kuwa ofisi hiyo imewasilisha maombi ya rufaa na kufafanua kuwa imelifanya hilo katika muda sahihi.
Kimataifa Blatter, Platini kushitakiwa upya
Blatter, Platini kushitakiwa upya
Related posts
Read also
