Na mwandishi wetu
Wachezaji wa Simba wameeleza kuwa licha ya ushindi walioupata ugenini lakini kuelekea mechi yao ya wikiendi hii ya marudiano dhidi ya Primiero de Agosto wataingia uwanjani wakiwa wanajua bado kuna kazi ya kufanya.
Simba Jumapili itaikaribisha de Agosto kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam baada ya mechi ya wikiendi iliyopita iliyopigwa Luanda, Angola na Simba kushinda kwa mabao 3-1.
Wekundu hao wanahitaji ushindi wa matokeo ya jumla ili kufuzu kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kiungo wa timu hiyo, Clatous Chama alisema kwamba anaamini yeye na wenzake wako tayari na wanafahamu umuhimu wa ushindi katika mchezo huo hivyo wataingia wakiwa na majukumu ambayo lazima wayakamilishe ndiyo wamalize mtihani walionao.
“Niko tayari na ninaamini hata wenzangu pia wako tayari, muhimu ni kufahamu tunataka nini kwenye hiyo mechi, tumecheza mechi ya kwanza Angola na tunajua matokeo lakini kikubwa ni kujua mechi bado haijamalizika, tuna kazi ya kufanya na tunaweza kuifanya, tutaingia kwenye mechi tunajua nini tunatafuta mpaka dakika 90 zitakapokamilika,” alisema Chama.
Naye beki wa timu hiyo, Joash Onyango alikumbushia kilichowatokea msimu uliopita walipokubali kutolewa na Jwaneng Galaxy ya Bostwana na kushindwa kucheza makundi hivyo amesisitiza kuongezeka kwa umakini siku hiyo, kama ambavyo pia amezungumza kiungo Jonas Mkude.
“Kutokana na umuhimu wa mchezo kila mchezaji amejiandaa vizuri kwa sababu matokeo ya Galaxy kila mmoja yalimuumiza kuanzia mashabiki, wachezaji, viongozi, benchi la ufundi lakini mwisho wa siku yale yamepita na tunaenda kwenye mechi hii tukiwa na tahadhari kubwa tukifahamu kwenye mpira chochote kinaweza kutokea lakini tumejiandaa vya kutosha,” alisema Mkude.
Msimu uliopita Simba ilijikuta ikidondokea kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushinda 2-0 ugenini dhidi ya Galaxy na kisha kufungwa mabao 3-1 nyumbani na hivyo Galaxy kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
Soka Wachezaji Simba: Kazi haijakamilika
Wachezaji Simba: Kazi haijakamilika
Related posts
Read also