Na mwandishi wetu
Wakati Yanga ikiendelea kujifua kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeelezwa kuwa wapinzani wao, Al Hilal wanatarajia kutua nchini kesho Alhamisi kwa ajili ya mchezo huo wa Jumamosi.
Yanga inakutana na Al Hilal kutoka Sudan baada ya ushindi wa jumla wa mabao 9-0 dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini kwenye raundi ya awali ya ligi hiyo.
Hilal inayonolewa na kocha Florent Ibenge ilipenya kwa bao la ugenini dhidi ya St George ya Ethiopia baada ya mechi ya awali kufungwa mabao 2-1 na kisha kuibuka na ushindi wa nyumbani wa bao 1-0.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ameeleza kwamba wamepewa taarifa na wapinzani wao hao kuwa wanatua kesho nchini huku akisisitiza kuwa watautumia mchezo huo kupata matokeo yatakayowarahishia kazi kwenye mechi ya marudiano Oktoba 16, mwaka huu.
Pia alisisitiza kuwa kwa sasa wapo kwenye kampeni kabambe kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ambayo mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 1998.
“Kwa taarifa ni kwamba Al Hilal wanaingia nchini siku ya kesho, kwa hiyo hakuna mabadiliko yoyote mpaka sasa na sisi kama Wananchi, kama Yanga tunajiandaa kuwapokea wapinzani wetu.
“Na siku zote tunafanyia kazi taarifa rasmi, kwa hiyo kama kuna kachero wao kama kuna mtu ametangulia kama Yanga hatuwezi kuangalia hayo mambo, sisi tuna timu nzuri inayojiandaa kwa mechi na Uwanja wa Mkapa utatoa majibu sahihi ya kitakachotokea,” alisema Kamwe.
Pia, Kamwe alieleza namna wachezaji wanavyohitaji ushindi katika mchezo huo na namna walivyopania kuhakikisha wanaipeleka Yanga kwenye ramani ya michuano hiyo kwa kufika mbali msimu huu.
“Tungependa mashabiki na wanachama waje kuujaza uwanja na kushangilia uwanja mzima kama uongozi wa Yanga ndiyo ombi letu, kama ilivyo kwa wachezaji ambao wanahitaji hamasa ya mashabiki kuhakikisha tunafanya vizuri na kwenda hatua ya makundi, rekodi ambayo wachezaji imekuwa ikiwaumiza na wamedhamiria Yanga icheze makundi safari hii,” alisema Kamwe.
Mchezo huo wa awali unatarajiwa kupigwa majira ya saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Soka Wapinzani wa Yanga kutua Dar Alhamisi
Wapinzani wa Yanga kutua Dar Alhamisi
Related posts
Read also