Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imemtangaza rasmi Mzambia, Andrew Mtine kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa klabu hiyo akirithi mikoba ya Senzo Mazingiza raia wa Afrika Kusini.
Yanga kupitia Rais wake, Hersi Said imemtangaza Mtine leo jijini Dar es Salaam sambamba na uzinduzi wa tovuti na programu tumishi ya timu hiyo kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano na wanachama pamoja na mashabiki wake.
Hata hivyo kilichoteka hisia za wengi ni saa chache baada ya utambulisho huo, Senzo kutoa pongezi kwa Mtine na kumkaribisha katika majukumu yake hayo mapya.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Senzo aliyeondoka Jangwani Julai 31, mwaka huu baada ya kumalizika kwa mkataba wake aliandika: “Karibu Mwananchi, kila la heri katika majukumu yako mapya Andre.”
Kihistoria tangu kuanza kwa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Yanga, Mtine anakuwa Mtendaji Mkuu wa pili kuiongoza klabu hiyo baada ya Senzo aliyedumu Yanga kwa miaka mitatu akitokea kwa mahasimu wao klabu ya Simba.
Akizungumza juu ya ujio wa Mtine aliyewahi kuhudumu kama mtendaji wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, Hersi alisema wamefurahi kumpata mtendaji wao huyo baada ya mchakato wa maombi uliopitiwa na kamati ndogo iliyopitia kwa kina na kumchagua Mtine.
Aidha, Mtine ambaye pia amewahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya Fedha ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) alieleza namna gani amefurahishwa kujumuika na timu hiyo na kwamba atashirikiana na uongozi pamoja na mashabiki kuipeleka mbali zaidi.
“Ni heshima kubwa kuwa mtendaji mkuu wa Yanga, kama alivyosema Rais kwamba Yanga ina historia kubwa na wanaouliza kwanini nipo hapa, niwaambie tu kwa sababu Yanga ni timu kubwa.
“Niwashukuru kwa mchango wa wote walioiunda Yanga mwaka 1935 na walioiongoza mpaka leo, mashabiki pia ni watu muhimu bila wao timu isingekuwa hapa, nimekuwa kwenye mpira miaka mingi lakini nafurahi kupata nafasi ya kufanya kazi Yanga,” alisema Mtine.
“Nimewahi kupita sehemu nyingi kama Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Zambia (ZAF), pia kama Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Nkana, nilipita Zesco kwenye benchi la ufundi kwa hiyo naamini kwa uzoefu nilionao kwa pamoja nikishirikiana na Rais na kamati nzima tutaipeleka hii klabu kwenye mafanikio makubwa Afrika,” alifafanua Mtine.
Soka Mzambia amrithi Senzo Yanga
Mzambia amrithi Senzo Yanga
Related posts
Read also