Paris, Ufaransa
Sakata la nyota wa Juventus, Paul Pogba na kaka yake Mathias Pogba limechukua sura mpya baada ya Mathias kuachia picha za video zaidi ya 30 zikimuonyesha ndugu yake na kundi la marafiki jinsi wanavyoishi maisha ya kifahari na namna ndugu yake huyo anavyoamini ushirikina.
Paul na Mathias wamekuwa katika ugomvi na tayari Paul amemfikisha ndugu yake katika vyombo vya sheria akimtuhumu kwa uzushi na vitisho vyenye lengo la kujipatia pesa kwa njia zisizo halali, Mathias na wenzake wanne walikamatwa Jumamosi iliyopita, kuhojiwa na kulala polisi kwa tuhuma hizo.
Haikuwekwa wazi ni lini hasa video hizo zilipigwa lakini Mathias aliwahi kuahidi kuweka wazi mambo mabaya ya ndugu yake kwa alichosema kwamba wakati umefika kwa ulimwengu kumfahamu vizuri Paul ni mtu wa aina gani. Wakili wa Mathias ambaye awali alisema mteja wake hana kosa lolote hakuweza kupatikana kuelezea undani wa picha hizo.
“Kama unaziangalia hizi video hivyo ndivyo zilivyo, kwa sababu ndugu yangu Paul Pogba amepata njia ya kuninyamazisha, nimerekodi hizi video kwa sababu kwa yote yaliyotokea kila kitu kinabainishwa wazi,” alisema.
Katika video hizo, Mathias anamtuhumu ndugu yake kwa kuwatelekeza ndugu wa faimilia yao na kuwaacha wakiishi katika umasikini lakini pia amemhusisha na matukio ya jinai na kurudia tuhuma alizotoa awali kwamba ndugu yake anamini katika ushirikina na ‘ameajiri’ mganga wa kienyeji ingawa hakuweza kutoa ushahidi wowote katika madai hayo.
Mathias mwenye miaka 32, pia katika tuhuma hizo anadai kwamba mganga wa kienyeji aliyeajiriwa na Paul yuko karibu na mwanasoka nyota wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Alou Diarra na Paul alitambulishwa kwa mganga huyo na beki wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG), Serge Aurier.
Alifafanua kuwa Paul kwa miaka kadhaa sasa amekuwa akitumia mamilioni kupata huduma ya mganga huyo, kwa mfano aliwahi kumtaka aisaidie Ufaransa ishinde Kombe la Dunia au walau awatoe mchezoni mapema wanasoka wa timu pinzani.
Mathias aliwahi kusema kwamba Paul amekuwa akimuwinda Kylian Mbappe ingawa hakufafanua ni kivipi badala yake alisema kwamba Paul aliwahi kumtaka mganga huyo ampunguzie makali Mbappe kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya PSG na Man United mwaka 2019, mechi ambayo United ilishinda kwa mabao 3-1 na kufuzu hatua ya robo fainali.
Katika hatua nyingine, Mathias pia amedai kwamba maisha yake yako hatarini kwa sababu ya Paul na tayari baadhi ya ndugu zake wamedhalilishwa na kushambuliwa.
Kwa sasa pamoja na tuhuma hizo, Polisi wa Ufaransa wanazifanyia kazi tuhuma za awali kwamba Paul anawindwa na genge la wazushi likiongozwa na Mathias na marafiki zake wa utotoni ambao wanataka wanyamazishwe kwa kulipwa na Paul, Euro 13 milioni, jambo ambalo Mathias amelikana.
Mathias naye ni mwanasoka ingawa kwa sasa hana timu, amewahi kuzichezea timu mbalimbali barani Ulaya na mara ya mwisho miezi mitano iliyopita alikuwa akiichezea klabu ya daraja la nne nchini Ufaransa ya Belfort.
Kimataifa Pogba adaiwa kuajiri mganga wa kienyeji
Pogba adaiwa kuajiri mganga wa kienyeji
Related posts
Read also