London, England
Kocha wa Brighton, Graham Potter amefanya mazungumzo ya awali na matajiri wa Chelsea na inadaiwa amekubali kujiunga na timu hiyo kuchukua nafasi ya Thomas Tuchel aliyetimuliwa jana.
Potter mwenye umri wa miaka 47, Jumatano usiku inadaiwa alifanya mazungumzo marefu na matajiri na wamiliki wa klabu ya Chelsea, Todd Boehly na Behdad Eghbali huku habari za ndani zikidai kwamba kocha huyo alikubali mambo mengi katika mazungumzo hayo.
Kocha huyo leo Alhamisi alitarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari lakini mkutano huo ulifutwa kwa kinachoaminika kuwa ni kupata nafasi ya kuwaaga wachezaji na maofisa wake kabla ya kwenda London, kusaini rami mkataba wa kuanza kazi ya kuinoa Chelsea.
Kwa mantiki hiyo, Potter huenda akawa uwanjani Jumamosi hii kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu England kati ya Chelsea na Fulham iwapo atakamilisha mambo yote ya msingi huku ikiaminiwa kwamba akiwa katika kazi yake hiyo mpya ataongozana na baadhi ya watu wake wa benchi la ufundi akiwamo msaidizi wake, Billy Reid.
Awali mara tu baada ya Tuchel kutimuliwa baadhi ya makocha waliotajwa kumrithi ni Mauricio Pochettino na Zinedine Zidane lakini baadaye ikaelezwa kwamba Potter ndiye aliyekuwa chaguo la kwanza la matajiri wa Chelsea hasa baada ya madai kwamba Zidane hana nia ya kuwa kocha wa timu yoyote ya England badala yake anaifikiria kazi ya kuinoa timu ya Taifa ya Ufaransa.
Jina la Potter limekuwa maarufu kutokana na kazi yake anayoifanya na klabu ya Brighton ambayo msimu uliopita ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya tisa na msimu huu ipo nafasi ya nne ikiwa tayari imejijengea heshima baada ya kuiadhibu Man United kwa mabao 2-0.
Kukamilika kwa dili la Potter katika klabu ya Chelsea maana yake ni kwamba klabu ya Brighton aliyojiunga nayo kwa mara ya kwanza mwaka 2019, itaneemeka kwa kulipwa fidia inayotajwa kufikia Pauni 16 milioni.
Kimataifa Potter akubali kumrithi Tuchel Chelsea
Potter akubali kumrithi Tuchel Chelsea
Read also
