Manchester, England
Mchambuzi wa soka na nahodha wa zamani wa Man United, Gary Neville anatarajia kufikishwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali kwa kuingilia uhuru wa mahakama katika kesi ya udhalilishaji kijinsia inayomkabili mchezaji mwenzake wa zamani wa klabu hiyo, Ryan Giggs katika Mahakama ya Manchester.
Giggs anatuhumiwa kumpiga kichwa aliyekuwa mpenzi wake, Kate Greville pamoja na matukio mengine ya udhalilishaji ambapo wakati kesi ikiendelea, Neville anadaiwa kutoa kauli kwenye mitandao ya kijamii, kauli ambazo mawakili wa upande wa mashitaka wanaziona kuwa ni kuingilia uhuru wa mahakama au mwenendo wa kesi.
Neville anadaiwa kutoa kauli ambazo zimetafsiriwa kama ni kuingilia uhuru wa mahakama na ingawa kauli hizo hazijawekwa wazi na vyombo vya habari lakini katika kujitetea kwake, Neville kupitia wakala wake alisema kwamba kauli hizo ziliilenga familia ya Glazer ambayo inamiliki klabu ya Manchester United na si kesi inayomkabili Giggs.
Kwa mujibu wa sheria ni marufuku kuingilia mwenendo wa kesi au uhuru wa mahakama iwe ni kwa kutoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii au kwa namna yoyote ile taarifa ambayo itaonekana kuwa na ushawishi au kuhusiana kwa namna yoyote na kesi inayoendelea na adhabu ya kosa hilo ni faini au kufungwa jela kwa miaka miwili.
Akizungumzia alichokifanya Neville, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Hilary Manley alisema kwamba ameamua kulifikisha suala hilo kwa mwanasheria mkuu wa serikali akizihusisha kauli hizo kuwa ni kuingilia uhuru wa mahakama au mwenendo wa kesi.
Ilielezwa mahakamani kwamba mtoaji wa kauli hizo ni mtu maarufu na akaunti yake ya Instagram inafuatiliwa na watu wapatao milioni 1.5 na alichokisema kinaonekana kutoa ushawishi katika kesi ya jinai inayomkabili Giggs na hivyo kutafsiriwa kuwa ni kuingilia mwenendo wa kesi au uhuru wa mahakama.
Giggs amekana mashitaka yote yanayomkabili ikiwamo ya kumpiga kichwa mkewe, kuwa mbabe na udhalilishaji wa kijinsi, matukio ambayo inadaiwa alikuwa akimfanyia Kate wakati wawili hao wakiwa wapenzi kabla ya kutengana.
Kutokana na kesi hiyo, Giggs alilazimika kujiuzulu ukocha wa timu ya Taifa ya Wales kwa kile alichodai kuwa ni kutotaka maandalizi ya timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia yaathiriwe kwa namna yoyote ile na kesi inayomkabili.
Kimataifa Kesi ya Giggs yamponza Gary Neville
Kesi ya Giggs yamponza Gary Neville
Read also
