New York, Marekani
Wanawake wawili wamemfikisha mahakamani bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, George Foreman wakimtuhumu kwa kuwabaka na kuwadhalilisha kijinsia, makosa ambayo wanadai aliwafanyia miaka ya 1970.
Katika madai hayo wanawake hao wamedai kwamba wote walikutana na bondia huyo wakiwa wadogo wakati huo baba zao wakiwa wameajiriwa na bondia huyo ambaye kwa sasa ana miaka 73.
Mwanamke mmoja katika madai yake alimtuhumu Foreman kwa kumlea akiwa na miaka minane na kuanza kufanya naye ngono akiwa na miaka 15 wakati mwenzake alidai kwamba Foreman alikuwa akimdhalilisha kijinsia na kumbaka akiwa na miaka 15 na 16. Foreman amekana tuhuma hizo.
Katika taarifa yake aliyoitoa Julai wakati tuhuma hizo zilipotangazwa hadharani, Foreman alisema, “Katika kipindi cha miezi sita iliyopita wanawake wawili wamekuwa wakijaribu kuvuna mamilioni ya dola kutoka kwangu na kwa familia yangu, wamekuja na madai ya uwongo wakidai kwamba niliwadhalilisha kijinsia miaka ya 1970, zaidi ya miaka 45 iliyopita.”
“Nazipinga na kuzikataa tuhuma hizi, heshima niliyojiwekea ina maana kubwa kwangu pamoja na mafanikio yangu kwenye michezo na siwezi kutishwa na vitisho vya uwongo na visivyo na msingi,” alisema na kuongeza, “siwezi kununua ugomvi lakini pia siwezi kuwakimbia.”
Wanawake hao ambao umri wao unafikia miaka 60 na zaidi kila mmoja kwa wakati wake aliwasilisha madai hayo Jumatano hii katika Mahakama ya Los Angeles akitaka kulipwa fidia.
Mmoja wa wanawake hao alisema kwamba Foreman alimtisha akimwambia kwamba baba yake atapoteza kazi ya kuwa mshauri wa ngumi wa bondia huyo kama asingekubaliana naye.
Foreman ni miongoni mwa mabondia maarufu wa Marekani, alijipatia umaarufu kwa kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki mwaka 1968 na kushinda mkanda wa uzito wa juu duniani mwaka 1973 kwa kumchapa mshindi asiyeshindika wa wakati huo, Joe Frazier na kuutetea mkanda huo mara mbili kabla ya kupigwa na Muhammad Ali mwaka 1974.
Ngumi Foreman kortini, adaiwa kubaka wanawake wawili mwaka 1970
Foreman kortini, adaiwa kubaka wanawake wawili mwaka 1970
Read also
