Helsinki, Finland
Usiku wa Jumatano umekuwa mzuri kwa Real Madrid baada ya kubeba taji la Uefa Super Cup ikiichapa Eintracht Frankfurt mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Olympic mjini Helsinki huku Karim Benzema akizidi kutajwa kwenye tuzo ya Ballon d’Or.
Uefa Super Cup ni mechi inayowakutanisha vinara wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambao ni Real Madrid dhidi ya vinara wa Europa Ligi ambao ni Frankfurt, na hivyo ushindi huo unawafanya Madrid wawe wamebeba taji jingine la Ulaya baada ya lile la Ligi ya Mabingwa.
Alikuwa ni David Alaba aliyeipatia Madrid bao la kwanza katika dakika ya 37 akiitumia vizuri pasi ya kichwa ya Casemiro na kuujaza mpira wavuni huku akimuacha kipa wa Frankfurt, Kevin Trapp akiwa ameduwaa kwa namna pasi ya Casemiro ilivyomkuta mfungaji.
Kinara wa mabao wa Madrid, Benzema aliandika bao la pili dakika 20 baada ya kuanza kipindi cha pili baada ya kuinasa krosi ya Vinicius Jr na kuujaza mpira wavuni kwa bao ambalo si tu liliihakikishia Madrid taji jingine la Ulaya bali pili liliiboresha rekodi ya jumla ya mabao ya Benzema.
Kwa sasa Benzema anakuwa ameshika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi katika klabu hiyo akiwa amempiku nahodha wa zamani wa timu hiyo, Raul Gonzalez huku akiwa ametanguliwa na Cristiano Ronaldo mwenye rekodi ya mabao 450.
Benzema ambaye alikuwa nahodha wa Madrid katika mchezo huo, kwa mafanikio hayo anazidi kutajwa katika mbio za kuwania Ballon d’Or, Oktoba mwaka huu akibebwa na taji la La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Hispania au La Liga na amemaliza msimu wa 2021/22 akiwa na jumla ya mabao 44 katika mechi 46 za mashindano mbalimbali.
Akiizungumzia nafasi ya Benzema kushinda Ballon d’Or, kiungo wa zamani wa England, Owen Hargreaves alisema ni mshambuliaji wa aina yake, “Kama hatoshinda Ballon d’Or msimu huu basi hatoshinda tena, na sioni ni kwa vipi asishinde, ni mchezaji wa kipekee, hata kama umri unakwenda lakini hilo litakuwa katika namna nzuri kwa sababu wakati wote amekuwa mchezaji makini.”
Kimataifa Madrid yabeba Super Cup, Benzema atajwa Ballon d’Or
Madrid yabeba Super Cup, Benzema atajwa Ballon d’Or
Read also
