Na mwandishi wetu
Bondia Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ ameibuka na kumueleza mpinzani wake, Shaban Kaoneka kuwa hapaswi kulalamika juu ya riziki anayoipata baada ya kumalizika kwa pambano lao kwani hiyo imetokana na kudra za Mungu mwenyewe.
Mandonga ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja imepita tangu Kaoneka alalamike kuwa vyombo vya habari havikumtendea haki kwa kutompa muda wa kumuhoji kama anaoupata Mandonga na mwishowe anaona alivyostahili kuvipata yeye kama mshindi wa pambano lao vinatua kwa Mandonga.
“Shabani ndugu yangu mimi naamini kabisa riziki inatoka kwa mafungu na kwa muda maalumu alioupanga Mungu, suala la nani afanikiwe nani aishie njiani ni majukumu ya Allah, mimi na wewe hatupaswi kumlaumu mtu yoyote yule.
“Katika tasnia hii ya mchezo wa ngumi na watu wa media kiujumla hata mimi sijawahi kuwaza kwamba ipo siku nitasimama kama ‘superstar’ mkubwa lakini yote kwa yote tujifunze kumshukuru Mungu kwa kila jambo. Kama ipo ipo tu,” alifafanua Mandonga.
Wawili hao walipigana mkoani Ruvuma wiki iliyopita kwenye pambano la utangulizi la ndondi zilizomshuhudia Selemani Kidunda akitwaa mkanda wa WBF kwa kumtandika Erick Tshimanga wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC).
Hata hivyo, pamoja ya Kaoneka kuibuka na ushindi lakini Mandonga ndiye aliyetawala kwenye vichwa vyua habari na mitandaoni, hiyo ikitokana na vituko alivyokuwa akivionesha bondia huyo kabla ya mchezo na mwisho wafuatiliaji wengi kutaka kufahamu kuhusu bondia huyo na mwisho sasa amekuwa maarufu akitajwa kupata dili mbalimbali kila kukicha.
Ngumi Mandonga amjibu Kaoneka
Mandonga amjibu Kaoneka
Read also
