Na mwandishi wetu
Sekretarieti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewafungulia mashitaka ya kimaadili, Rais wa Yanga, Hersi Said na msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara ambaye kwa sasa anatumikia adhabu ya kufungiwa kwa miaka miwili.
Kamati ya Maadili ya TFF hivi karibuni ilimfungia Manara kujihusisha na shughuli za soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili pamoja na kumtoza faini ya Sh 20 milioni ambapo TFF wanadai Manara ameshindwa kutekeleza adhabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyopatikana leo na kusainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, Clifford Ndimbo, ilieleza kuwa Hersi anadaiwa kwenda kinyume na Ibara ya 16 ya Katiba ya TFF pamoja na Ibara ya 1 ya Katiba ya Yanga.
Ndimbo katika taarifa yake alifafanua kwamba baada ya Manara kuadhibiwa, TFF ilimuandikia barua Hersi akiwa ndiye kiongozi wa Yanga ili kuhakikisha klabu yake inaheshimu uamuzi huo wa Kamati ya Maadili dhidi ya Manara.
Tayari TFF imepeleka mashitaka hayo kwa mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ili walalamikiwa waelezwe mashitaka yao na hatimaye kuitwa wakati wowote kamati hiyo itakapopanga tarehe ya kusikiliza mashitaka hayo.
Taarifa ya TFF ingawa haikueleza ni vipi Manara ameshindwa kutekeleza adhabu aliyopewa lakini inadhaniwa kwamba kitendo chake cha kuwapo kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi jana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam huenda kimetafsiriwa kuwa ni kujihusisha na masuala ya soka.
Manara hata hivyo akiwa katika sherehe hizo alishiriki kutambulisha wachezaji ambapo alisema kwamba ameshiriki kama MC wa shughuli kutoka Kigogo, Sambusa jijini Dar es Salaam.
Manara alifungiwa na kamati hiyo ya TFF baada ya mzozo kutokea baina yake na Rais wa TFF, Walace Karia, mzozo uliotokea Julai 2 mwaka huu kwenye Jukwaa Kuu la Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha wakati wa mechi ya fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Costala Union.
Katika tukio hilo Manara anadaiwa alimshambulia Karia kwa kumwambia: “Wewe unanifuatafuata sana na hii ni mara ya tatu, sikuogopi kwa lolote nina uwezo wa kukufanya lolote na huna uwezo wa kunifanya lolote.”
Manara hata hivyo baadaye aliomba radhi kwa tukio hilo ingawa Kamati ya Maadili ya TFF iliendelea kusikiliza shauri hilo na hatimaye kumchukulia hatua.
Soka Manara, Hersi wafikishwa Kamati ya Maadili
Manara, Hersi wafikishwa Kamati ya Maadili
Read also
