Manchester, England
Katika hali ambayo haikutarajiwa, kocha Erik ten Hag amesema si sahihi kumsakama Cristiano Ronaldo peke yake kwa kutoka nje kabla ya mechi ya Man United na Rayo Vallecano wakati kuna wachezaji wengine waliofanya hivyo.
Ronaldo katika mechi hiyo alicheza kwa dakika 45 za kwanza na kutolewa lakini akatoka uwanjani dakika 10 kabla ya mechi kumalizika na ingawa wako wachezaji wengine waliotoka, Ronaldo amejikuta akisakamwa zaidi yeye kwenye vyombo vya habari na kukawa na taarifa kwamba Ten Hag hatompanga katika mechi ya kwanza ya Man Utd ya Ligi Kuu England hapo kesho dhidi ya Brighton.
Akifafanua kuhusu kusakamwa kwa mchezaji huyo, Ten Hag alisema si sahihi kumuangalia Ronaldo peke yake na kuwaacha wachezaji wengine waliotoka uwanjani mapema katika mechi hiyo ya kirafiki iliyopigwa kwenye dimba la Old Trafford na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
“Na sasa ninachotaka kusema ni kwamba waliotoka uwanjani kabla ya mechi walikuwa wachezaji wengi lakini anayeangaliwa ni Cristiano, hiyo si sahihi, kwa hiyo mkafanye utafiti na mtaona ni wachezaji wengi waliotoka,” alisema Ten Hag jana jioni.
“Watajeni, wasahihisheni na baada ya hapo endeleeni na mengine, nafikiri nimesema ya kutosha kuhusu hilo, si sahihi,” alisisitiza Ten Hag.
Ronaldo ambaye hakuwamo katika ziara ya maandalizi ya msimu wa 2022/23 katika nchi za Thailand na Australia na kukosa mechi kadhaa za kirafiki, amecheza mechi moja tu kwa dakika 45 huku ikidaiwa kwamba hayuko fiti lakini huenda akapangwa katika mechi ya kesho baada ya Anthony Martial kuumia.
Akizungumzia maandalizi ya timu yake kwa ujumla kwa ajili ya mechi ya kesho, Ten Hag alisema, “Nimeridhishwa na timu yote, tunafanya vizuri, hali ni nzuri na Cristiano anafanya bidii sana, nina furaha kuwa naye, nilishasema kabla tuna mshambuliaji wa kiwango cha juu, hakika nina furaha yuko hapa katika kikosi, na tunasimamia mipango yetu.”
Habari za ndani zinadai kuwa Man Utd bado inahaha kusajili kiungo na mshambuliaji kabla ya siku ya mwisho ya usajili ambayo ni Septemba mosi, hawajakata tamaa kwa Frankie de Jong, kiungo wa Barcelona ambaye pia anatakiwa na Chelsea ingawa Ten Hag hakutaka kumzungumzia mchezaji huyo kwa madai kwamba hayuko tayari kuzungumzia mchezaji mwenye mkataba na timu nyingine.
Kimataifa Ten Hag: Msimsakame Ronaldo
Ten Hag: Msimsakame Ronaldo
Read also
