Milan, Italia
Kiungo wa zamani wa Arsenal na Barcelona, Cesc Fabregas amejiunga na klabu ya Como 1907 ya Italia inayocheza ligi ya Serie B kwa mkataba wa miaka miwili huku ikiamini atakuwa msaada kwa timu hiyo kufuzu kucheza Serie A.
Fabregas, kiungo mwenye umri wa miaka 35 sasa ambaye pia amewahi kuichezea timu ya Taifa ya Hispania, amejiunga na Como akiwa mchezaji huru, mara ya mwisho Januari 2019 alisajiliwa na Monaco ya Ufaransa akitokea Chelsea wakati huo kocha wa Monaco akiwa ni Thiery Henry ambaye ni mchezaji mwenzake wa zamani wa Arsenal.
“Nimekuwa mwenye bahati kwa sababu katika maisha yangu ya soka nimepata nafasi ya kucheza katika klabu zenye sifa za kipekee, na katika hilo Como haiwezi kuwekwa kando, sina cha kusubiri zaidi ya kuingia uwanjani mbele ya mashabiki katika mazingira haya yanayovutia,” alisema Farbregas.
“Utamaduni wa klabu hii na shauku ya wamiliki kuifikisha katika hatua ya juu ni sababu inayotia hamasa na kwa sababu hiyo nasubiri kwa hamu kuanza kucheza,” aliongeza.
Ofisa mtendaji mkuu wa klabu ya Como, nyota wa zamani wa Chelsea na timu ya Taifa ya England, Dennis Wise, alimkaribisha Fabregas ambaye pia ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha Hispania kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
“Mchezaji ambaye amefanya mengi katika historia ya soka na ambaye sasa atakuwa mtu muhimu katika mipango na matarajio ya Como, mchezaji wa aina hii na mwenye uzoefu ni muhimu katika mipango yetu ya miaka mitatu kufuzu na kucheza Serie A,”alisema Wise.
Fabregas ameichezea Monaco mechi 68 katika miaka mitatu na nusu aliyokuwa na klabu hiyo ingawa aliandamwa na majeraha msimu uliopita, akiwa Arsenal kuanzia mwaka 2004 hadi 2011 amecheza mechi 212 kabla ya kujiunga na Barcelona, klabu ambayo awali ilimsajili mwaka 1997 akiwa na miaka 10. Baada ya kuichezea Barcelona, mwaka 2014 aliihama timu hiyo na kujiunga na Chelsea.
Kimataifa Fabregas aibukia Serie B Italia
Fabregas aibukia Serie B Italia
Related posts
Read also
