Fenerbahce, Uturuki
Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) linachunguza tukio la mashabiki wa soka wa timu ya Fenerbahce ya Uturuki waliokuwa wakishangilia kwa kulitaja jina la Rais wa Urusi Vladmir Putin baada ya timu yao kufungwa mabao 2-1 na Dynamo Kiev ya Ukraine katika mechi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tukio la kushangilia na kuzomea huku likitajwa jina la Putin linahisiwa kuhusishwa na uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Urusi nchini Ukraine hadi kusababisha Urusi kufungiwa kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar Novemba mwaka huu.
Maelfu ya mashabiki wa Fenerbahce walianza zomea zomea hiyo baada ya timu yao kufungwa goli ikiwa tayari imetoka sare ya 0-0 katika mechi ya kwanza ambayo ililazimika kuchezwa nchini Poland kwa kuwa hali ya usalama nchini Ukraine si nzuri kutokana na uvamizi wa Urusi uliosababisha vita baina ya nchi hizo mbili. Kwa matokeo hayo Fenerbahce, timu anayoichezea Mtanzania Mbwana Samatta, imepoteza nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa.
Kiungo Vitaliy Buyalskyi ndiye aliyeipatia Dynamo bao la kuongoza katika dakika ya 57, bao ambalo linadaiwa kuwa chanzo cha balaa hilo lakini Fenerbahce walifanikiwa kusawazisha na timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya 1-1 kabla Dynmo haijapata bao la pili katika dakika ya 114 lililofungwa na Oleksandr Karavaev.
Balozi wa Ukraine nchini Uturuki Vasyl Bodnar alisema tukio hilo limemsikitisha sana, “Hatuwezi kuelewa kunapokuwa na neno la kumuunga mkono muuaji na mvamizi kutoka Urusi ambaye kwa makusudi kabisa ameamua kuwaua watu wa Ukraine na kuiteketeza nchi yetu, hata soka mchezo ambao unapendwa nchini Uturuki ni lazima kuwe na mipaka.”
Zomea zomea na shangilia hiyo inaamika kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na bao alililofunga Buyalskyi ambaye inadaiwa baada ya kufunga bao hilo alishangilia kwa kutoa ishara inayoaminika kuiunga mkono timu ya Besiktas pia ya Uturuki ambao ni mahasimu wakubwa wa Fenerbahce.
Klabu ya Fenerbahce hata hivyo ilijitenga na tukio la mashabiki hao kwa madai kuwa haliwakilishi hisia za klabu au wajibu wake kwa jamii. “Kwa mara nyingine tunapenda kuukumbusha umma msimamo wetu, michezo na siasa wakati wote lazima vitenganishwe,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
Taarifa hiyo pia ilieleza kwamba zomea zomea hiyo ilidumu kwa sekunde zisizopungua 20 lakini zilianza upya chanzo kikiwa ni wachezaji wa Daynamo waliokuwa wakishangilia goli lao.
Kocha wa Dynamo, Mircea Lucescu aliwaambia waandishi wa habari baada tu ya mechi hiyo kwamba kwenye michezo tabia ya aina hiyo ya mashabiki haiwezi kukubalika. “Sikutegemea uzomeaji wa aina hiyo, inasikitisha,” alisema Lucescu ambaye amewahi kuwa kocha wa tmu ya Taifa ya Uturuki na baada ya hapo alikataa kushiriki mkutano na waandishi wa akionyesha kukerwa na mashabiki hao.
Tukio hilo limeamsha hisia za watu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wao wakitaka timu ya Fenerbahce ifungiwe kushiriki michezo Ulaya.
Uefa imeahidi kufanya uchunguzi kupitia kamati yake maadili dhidi ya klabu ya Fenerbahce na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baadaye na shirikisho hilo.
Februari 24 mwaka huu, Urusi iliivamia kijeshi Ukraine, tukio ambalo limekuwa likilaaniwa na mataifa mbalimbali duniani kote.
Kimataifa Mashabiki Fenerbahce matatani kwa kumtaja Putin
Mashabiki Fenerbahce matatani kwa kumtaja Putin
Related posts
Read also
