Na mwandishi wetu
Baada ya ngojangoja ya muda mrefu, hatimaye bondia wa Tanzania, Hassan Mwakinyo ametajwa kurejea ulingoni kuzichapa na Liam Smith, pambabo litakalofanyika Septemba 3, mwaka huu.
Mwakinyo atapigana na Smith ambaye ni bondia wa England kwenye pambano hilo linalotajwa kuwa la ubingwa wa dunia wa uzito wa super welter likiwa na raundi 12 na litafanyika jijini Liverpool, England.
Smith ni bondia namba moja Uingereza akishika nafasi ya sita duniani kwenye uzito huo huku akiwa na nyota tano, atapambana na Mwakinyo anayeshika nafasi ya 37 kwa sasa baada ya kuporomoka hivi karibuni na kuwa na nyota tatu na nusu.
Mwakinyo ambaye ameshuka kutokana na kutopanda ulingoni kwa muda mrefu, hata hivyo akishinda pambano hilo ataandika historia mpya zaidi ya ile ya mwaka 2018 alipomchapa bondia namba nane wa dunia, Sam Eggington na kupanda hadi ya nafasi ya 14 ya uzani huo duniani.
Mara ya mwisho, Mwakinyo anayeishi Florida, Marekani kwa sasa, alipigana Septemba, mwaka jana na kutetea ubingwa wa Afrika (ABU) kwa kumtandika Julius Indongo kwa ushindi wa TKO.
Upande wa Liam, yeye aliutetea mkanda wake huo Aprili mwaka huu kwa kumchapa Jessie Vargas kwenye Ukumbi wa Madison Square jijini New York, Marekani.
Imeelezwa kuwa pambano hilo litaoneshwa mubashara na kituo kikubwa cha Sky Sports siku hiyo huku baadhi ya mapambano ya utangulizi yakiwa ni baina ya bingwa wa Uingereza katika uzito wa light-heavyweight, Dan Azeez atakayezichapa na Shakan Pitters.
Ngumi Mwakinyo ulingoni Septemba
Mwakinyo ulingoni Septemba
Read also
