Barcelona, Hispania
Wakati akiwa na wasiwasi kuhusu hatma yake PSG, nyota wa timu hiyo, Neymar amejikuta katika majanga mengine baada ya kudaiwa kuwa uhamisho wake kutoka klabu ya Santos kwenda Barcelona ulitawaliwa na rushwa na ubadhirifu na tayari amefikishwa mahakamani.
Neymar alisajiliwa na Barcelona miaka tisa iliyopita akitajwa kuwa mmoja wa wanasoka wa Brazil wenye vipaji kwa sasa anaichezea PSG huku akiwa njia panda kama ataendelea kuichezea timu hiyo msimu wa 2022/23 au ataondoka wakati huo huo akiwa na kazi nyingine ya kukabiliana na tuhuma za ubadhirifu na rushwa katika mahakama ya Barcelona.
Shauri la Neymar linatarajia kuanza kusikilizwa mahakamani kuanzia Oktoba 17 ambapo watuhumiwa wengine katika sakata hilo ni marais wa zamani wa klabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu na Sandro Rosell, wazazi wa Neymar baba na mama yake na kampuni ya familia hiyo ya N&N pamoja na kocha wa zamani wa Santos, Odilio Rodrigues.
Watuhumiwa wote katika kesi hiyo wamekana tuhuma hizo zilizowasilishwa na taasisi moja inayojihusha na masuala ya uwekezaji ya DIS ambayo ilidai kuwa na haki ya kulipwa asilimia 40 ya ada ya uhamisho wa Neymar kutoka Santos kwenda Barcelona mwaka 2013
DIS ilidai kuwa pesa waliyolipwa ni chini ya ile waliyotakiwa kupata kama sehemu ya ada ya uhamisho wakati Neymar akisajiliwa na Barcelona ambapo ilielezwa kuwa ada yake ilifikia Euro 57.1 milioni lakini DIS walilipwa Euro 6.8 milioni kati ya Euro 17 milioni walizopewa Santos. DIS wanadai kuwa ada halisi ya uhamisho ilikuwa kubwa zaidi.
Ada za uhamisho wa Neymar kwa kipindi kirefu uhalali wake umekuwa katika matatizo, mwaka jana Barcelona ililazimika kumaliza nje ya mahakama shauri la mchezaji huyo kuhusu uhamisho wake ulioweka rekodi ya Euro 222 milioni kwenda PSG mwaka 2017. Wakati huo klabu ya Barcelona ilidai kuwa mchezaji huyo alilazimika kuwalipa mamilioni ya Euro alizolipwa wakati anasaini mkataba mpya na timu hiyo mwaka 2016.
Mwaka 2016, kwenye mahakama moja ya Barcelona, katika kesi iliyobatizwa jina la Neymar 1, klabu ya Barcelona ililazimika kulipa faini ya Euro 5.5 milioni katika mamlaka za Hispania kwa sababu ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria uliotawaliwa na uhamisho wa mchezaji huyo.
Mwaka 2014, Sandro Rosell alilazimika kujiuzulu urais wa klabu ya Barcelona wakati uchunguzi ukifanywa kuhusu uhamisho wa wachezaji, pia aliwahi kutupwa rumande kwa miezi 20 ingawa baadaye alionekana hana hatia katika kesi ya utakatishaji fedha iliyohusu haki za matangazo mwaka 2019.
Soka Neymar afikishwa mahakamani
Neymar afikishwa mahakamani
Read also
