Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Coastal Union ya Tanga leo imetambulisha wachezaji watatu wapya wanaomudu nafasi tatu tofauti uwanjani akiwamo kiungo kutoka nchini Benin lengo likiwa ni kujiweka sawa kuelekea msimu ujao wa 2022/23.
Coastal imeweka wazi kunasa saini ya kiungo mshambuliaji, Djibril Olatoundji kwa mkataba wa miaka miwili huku ikidaiwa kwamba mchezaji huyo ametoka katika klabu ya ASVO Benin ya nchini Benin anakotoka mchezaji huyo.
Mwingine aliyetambulishwa ni mshambuliaji kutoka KVZ ya Zanzibar, Maabad Maulid ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya kufanya vizuri akiwa Zanzibar na kuibuka mfungaji bora kwa misimu miwili mfululizo iliyopita.
Wagosi wa Kaya hao pia wamemnasa kipa wa timu ya taifa ya Comoro, Mahmoud Mroivili na sasa kufanya idadi ya makipa kutoka Comoro kuwa wawili kwenye Ligi Kuu Bara baada ya awali Azam kumtambulisha Ali Ahmada kutoka taifa hilo pia.
Mbali na wachezaji hao, pia Coastal inatajwa kumalizana na beki wa kati, Khatib Kombo kutoka Kipanga FC ya Zanzibar, kiungo mshambuliaji wa KMKM, Optatusy Lupekenya na mshambuliaji Omar Mbrauku kutoka Fountain Gate.
Msimu uliopita Coastal ilionesha ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu Bara wakimaliza nafasi ya saba licha ya kuyumba mwanzoni mwa ligi huku ikitinga fainali ya Kombe la FA ikipoteza kwa matuta 4-1 dhidi ya Yanga baada ya sare ya 3-3 ya dakika 90, hivyo sasa timu hiyo inaonekana kujipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao.
Soka Coastal yasajili kiungo wa Benin
Coastal yasajili kiungo wa Benin
Read also
