Na mwandishi wetu
Mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC wameeleza kuwa wanatarajia kuanza maandalizi ya msimu ujao rasmi Jumapili hii wakiwa na wachezaji 19 kabla ya wengine kuungana nao baadaye.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ameeleza hayo akifafanua kuwa watalazimika kuwakosa wachezaji wao wengine wanane katika siku za awali za maandalizi hayo kutokana na kuwepo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Pia, amesema kwamba kambi yao hiyo iliyopo Avic Town, Kigamboni wamepanga iwe na tija na matokeo bora kuelekea msimu ujao wa 2022/23 ili kuhakikisha wanatetea makombe waliyochukua kwenye msimu uliomalizika hivi karibuni wa 2021/22 na kuweka tija kwenye mapambano yao ya Klabu Bingwa Afrika.
“Tunakwenda kuanza msimu mwingine, tuna malengo pia na matazamiao ya kuhakikisha kwamba tunatwaa mataji yote matatu na pengine iwe zaidi ya hapo lakini pia ni msimu ambao tumeazimia kufika mbali michuano ya kimataifa tuwe na ushiriki ambao una tija.
“Tayari vijana wameshaanza kuingia kambini, tunaamini mpaka kufikia mwisho wa wiki hii yaani Jumapili kikosi kitakuwa tayari kwa ajili ya kuanza maandalizi, maana yake tutakuwa na wachezaji 19 ukiondoa wale nane ambao wapo kwenye majukumu ya Taifa Stars.
“Wale 19 wataanza program ya mwalimu na hawa waliopo timu ya taifa wataendelea na program na baada ya hapo watajumuika na wengine kuwa na kikosi cha wachezaji 27 tayari kwa kuendelea na maandalizi hayo,” alisema Bumbuli.
Bumbuli pia alisema kuwa kambi ya Kigamboni itawasaidia zaidi wachezaji wao kuzoea mazingira ya hali ya hewa ya Tanzania ambayo haitofautiani sana kimaeneo kulingana na mikoa ambayo ligi itachezwa na hiyo itakuwa faida nyingine kuelekea msimu ujao.
Msimu uliopita, Yanga ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kupita misimu minne, Kombe la FA na Ngao ya Jamii.
Soka Kambi Yanga kuanza Jumapili
Kambi Yanga kuanza Jumapili
Related posts
Read also