Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Azam imetangaza rasmi kufunga usajili wake kuelekea msimu ujao wa 2022/23 baada ya kumtambulisha beki wao mpya wa kati, Malickou Ndaye, 22 ambaye ni raia wa Senegal.
Azam imetangaza taarifa hizo leo na kufafanua kuwa imempa mkataba wa miaka mitatu mchezaji huyo kutoka Tungueth FC inayoshiriki Ligi Kuu Senegal baada ya kuridhishwa na kiwango alichokionesha katika msimu uliomalizika hivi karibuni.
Kwa usajili huo Azam sasa imesajili jumla ya wachezaji tisa kuelekea msimu mpya kwa ajili ya ushindani wa Ligi Kuu ya NBC, Kombe la Azam (ASFC) pamoja na na Kombe la Shirikisho Afrika.
Nyota wengine iliowanasa ni kipa wa kimataifa wa Comoro, Ali Ahmada, beki wa kulia Nathaniel Chilambo kutoka Ruvu Shooting, kiungo mkabaji Mnigeria Isah Ndala kutoka Plateau FC.
Wachezaji wengine ni viungo washambuliaji Tape Edinho (ES Bafing) na Kipre Junior (Sol FC) raia wa Ivory Coast, Mghana James Akaminko kutoka Great Olympic na wazawa Cleophace Mkandala (Dodoma Jiji) na Abdul Sopu aliyetokea Coastal Union.
Azam yenye maskani yake Chamazi jijini, Dar es Salaam imeeleza kuwa sasa inageukia rasmi maandalizi ya msimu ujao baada ya kumalizana na masuala ya usajili wakiwa wameanza mazoezi leo, wakitarajia kupaa kuelekea Misri Ijumaa hii kwa ajili ya kambi ya maandalizi hayo na kurejea nchini Agosti 12, mwaka huu.
Pia, Azam imeamua kuliongezea nguvu benchi lake la ufundi kwa kumuongeza kocha wa washambuliaji, Kali Ongala ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga na Kajumulo FC na ambaye aliwahi kuwa kocha wa timu hiyo miaka ya nyuma.
Wengine ni kocha wa makipa Dani Cadena na kocha wa viungo Mikel Guillen ambao wanatokea nchini Hispania na hivyo kukamilisha jeshi lao kamili kwa ajili ya msimu ujao. Msimu uliopita, Azam ilishika nafasi ya tatu nyuma ya vinara Yanga na Simba iliyoshika nafasi ya pili.
Soka Beki Msenegali afunga usajili Azam
Beki Msenegali afunga usajili Azam
Related posts
Read also
