Budapest, Hungary
Kiungo wa Arsenal, Declan Rice amesema ameumizwa baada ya kushindwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini anajivunia yeye na wachezaji wenzake kwa kufikia hatua ya fainali.
Arsenal ilishindwa kutamba katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya PSG kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida na 30 za nyongeza mechi iliyochezwa Jumamosi Mei 30, 2026.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England walikuwa na matumaini makubwa ya kubeba taji hilo ikiwa ni mara yao ya kwanza kufikia hatua ya fainali ya michuano hiyo mikubwa ya klabu tangu wafanye hivyo mara ya mwisho mwaka 2006.
Rice alisema inaumiza na kukatisha tamaa unapolikosa taji la Ligi ya Mabigngwa Ulaya katika hatua ya fainali kwa mikwaju ya penalti.
“Tunajaribu kuchukua mitazamo mingi kwa kuzingatia hatua kubwa tuliyofikia tukiwa timu, ni msimu wa kipekee, hii mechi yetu ya mwisho ni ya 63 katika michuano yote, tulijitoa kwa kila kitu hadi hatua hii tuliyofikia,” alisema Rice.
Rice alisema waliifikisha mechi kwenye hatua ya penalti na aliifahamu hatua hiyo ni kamari lakini anaamini katika soka ni unashinda au unashindwa kwenye penalti, na zipo timu bora ambazo zimepoteza mechi kwenye penalti katika fainali.
Alisema wao Arsenal wapo katika kundi lililoshindwa lakini cha msingi ni kwamba wameshinda pamoja na kushindwa pamoja.
Rice aliongeza kwa kusema kuwa ingawa ameumizwa lakini akikumbuka jinsi walivyouanza msimu mwezi Julai na hadi walipofikia sasa kila kitu kinaonesha kuwa ilikuwa safari nzuri ya msimu.
