Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba inaamini kuwa mechi na mahasimu wao wa jadi, Yanga maarufu Derby ya Kariakoo ndiyo iliyobeba hatma ya timu hiyo kubeba taji la Ligi Kuu NBC msimu huu wa 2025-26.
Simba na Yanga zitaumana Jumapili Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, mechi inayochezwa baada ya timu hizo kukutana Jumatano Aprili 29, 2026 kwenye fainali ya Kombe la Muungano na Simba kutoka na ushindi wa bao 1-0.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa mechi hiyo ndiyo itakayoamua ubingwa wa msimu huu kwa Simba kuupata au kuukosa hivyo ni lazima kwao kushinda.
“Hii ni ‘must win game’ (mechi ya lazima kushinda) ili tuweze kuchukua alama tatu na libaki gepu la alama mbili,” alisema Ally.
Ally pia alisema wachezaji wote walioumia na kutolewa katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano, Anicet Oura, Yusuf Kagoma na Kibabage wapo tayari kwa mchezo wa Jumapili.
Meneja habari huyo pia aliweka bayana kuwa mechi hiyo ni ngumu kwani hata mpinzani wao Yanga hatakubali kupoteza mechi mara mbili katika kipindi kisichozidi wiki moja wakati dhamira ya Simba ni kuona furaha yao inadumu.
“Tumeshawapasua na wanataka ushindi ili wapate amani, lakini hatupo tayari kuwa na furaha ya siku tatu pekee, tunataka furaha yetu idumu milele na furaha inadumu vipi, ni kwa kushinda mchezo wa Mei 3,” alisema Ally.
Kuhusu mechi kupelekwa kwenye Uwanja wa Isamuhyo unaolalamikiwa na baadhi ya mashabiki kuwa ni mdogo na hauna hadhi ya kubeba mechi kubwa kama hiyo Ally alisema lengo lao si kumkomoa mtu.
Ally badala yake alidai kuwa wanafahamu Uwanja wa Mkapa ni bora lakini kutokana na marekebisho yanayoendelea wameamua kuchagua Uwanja wa Isamuhyo kwa kuwa una eneo bora la kuchezea.
“Ukiacha Uwanja wa Mkapa, uwanja mwingine unaoongoza kwa eneo zuri la kuchezea ni Uwanja wa Isamuhyo,” alifafanua Ally.
Ally pia aliwahimiza mashabiki na wanachama wa Simba kununua tiketi zao mapema kwenye vituo husika na ambaye hatonunua tiketi asifike kwenye eneo la uwanja huo badala yake aangalie mechi hiyo ‘live’ kupitia Azam TV.
