Vancouver, Canada
Rais wa Fifa, Gianni Infantino amesisitiza kwa mara ya pili kuwa Iran itashiriki fainali za Kombe la Dunia na kucheza mechi zake nchini Marekani kama ilivyopangwa kwa mujibu wa ratiba ya awali.
Kauli ya rais wa Fifa imekuja kwa mara ya pili baada ya kuwapo habari kuwa ujumbe wa Iran ulizuiwa kuingia katika mkutano mkuu wa Fifa nchini Canada ingawa taaifa ya wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilidai kuwa kuzuiwa huko halikuwa jambo lililokusudiwa.
Habari za Alhamisi Aprili 30, 2026, zilidai kuwa wajumbe wawili wa Iran waliruhusiwa kuingia Canada lakini wakagoma kuingia katika mkutano baada ya mwenzao mmoja kukwama sababu ikiwa ni tatizo lililohusisha idara ya uhamiaji nchini humo.
Ilidaiwa kuwa maofisa wa Fifa walitaka Iran wawepo kwenye mkutano huo licha ya tatizo la mwenzao na idara ya uhamiaji lakini wakati wa ukaguzi wa washiriki, ilibainika kuwa ujumbe wa Iran haukuwapo kwenye ukumbi wa mkutano.
Kwa upande wake Infantino licha ya utata huo alisisitiza kwamba Iran itashiriki fainali za Kombe la Dunia kwa sababu ni jukumu lake kuwaleta watu pamoja na kuleta umoja.
“Ukweli ni kwamba Iran watashiriki fainali za Fifa za Kombe la Dunia 2026, watacheza mechi zao Marekani, sababu ya hilo ni rahisi tu marafiki zangu, ni kwa sababu lazima tuwe wamoja,” alisema Infantino.
Baadaye Rais wa Marekani, Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba kama Infantino hana tatizo na Iran kushiriki fainali za Kombe la Dunia na yeye Trump hana tatizo katika hilo.
Kauli hiyo ya Trump ni tofauti na kauli yake ya awali aliposema kwamba anaikaribisha timu ya Iran nchini Marekani kushiriki fainali za Kombe la Dunia lakini hawezi kuwahakikishia usalama.
Tangu kuibuka kwa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, imekuwapo hofu ya Iran kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza mapema mwezi ujao katika nchi za Marekani, Canada na Mexico hadi taifa hilo kutoa sharti la kutaka mechi zao zihamishiwe nchi nyingine.
