Na mwandishi wetu
Simba hatimaye imefuta unyombe mbele ya hasimu wake Yanga kwa kuilaza bao 1-0 katika mechi ya faianli ya Kombe la Muungano iliyopigwa Jumatano Aprili 29, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Bao hilo pekee lililoitoa kimasomaso, Simba lilipatikana katika dakika ya 119 mfungaji akiwa ni Salum Mwalimu kwa mkwaju wa penalti na hivyo kufuta unyonge wa Simba kunyanyaswa na Yanga tangu Agosti, 2023.
Mwalimu aliingia dakika ya 26 akichukua nafasi ya Anicet Oura aliyeumia na baada ya kuingia, mchezaji huyo alianza kuonesha uwezo wake akiwa ametoka kutamba kwa mabao katika mechi za awali za Simba za michuano hiyo dhidi ya Mlandege na Mafunzo.
Kwa kiasi kikubwa mechi hiyo ilitawaliwa na ushindani wa hali ya juu ingawa kila timu ilicheza kwa tahadhari kubwa na kutengeneza nafasi chache na haikushangaza kumaliza dakika 90 bila bao.
Hali iliendelea kuwa hivyo katika dakika 30 za nyongeza kiasi cha kuibua matarajio ya timu kumaliza dakika 120 bila kufungana na hatimaye kuingia katika penalti tano tano kabla ya bao la Mwalimu kubadili matokeo.
Bao hilo lilitokana na penalti ambayo mwamuzi wa mchezo huo, Dickes Nyagrowa aliipa Simba baada ya Clatous Chama kuangushwa na Edmund John katika eneo la penalti.
Ushindi huo unaifanya Simba kuweka rekodi ya kubeba taji hilo kwa mara ya saba na hivyo kufungana na mahasimu wao Yanga ambao wamekuwa wakitambia rekodi hiyo.
Soka Simba yaizamisha Yanga, yabeba taji la Muungano
Simba yaizamisha Yanga, yabeba taji la Muungano
Read also
