Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi Yanga wamefuzu hatua ya fainali ya Kombe la Muungano baada ya kuichapa Azam FC mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa Jumamosi Aprili 25, 2026 kwenye dimba la New Amaan Complex, Zanzibar.
Yanga ilianza kuziona nyavu za Azam katika dakika ya sita kwa bao lililofungwa na mshambuliaji wa timu hiyo kutoka Zimbabwe, Prince Dube akitumia pasi ya Alan Okelo.
Kasi ya Yanga kusaka bao la pili ilizaa matunda katika dakika ya 25 kwa bao lililofungwa na kiungo wao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Maxi Nzengeli aliyeitumia pasi ya Dube kufunga bao hilo.
Bao pekee la Azam lilifungwa na Feisal Salum au Fei Toto katika dakika ya 77, bao ambalo alilifunga akinufaika na makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga waliochelewa kuokoa mpira katika eneo lao.
Kwa ushindi huo Yanga inasubiri kuumana na mshindi wa mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Simba na Mlandege ambayo itachezwa Jumapili Aprili 26 saa mbili usiku kwenye uwanja huo huo.
Mechi ya fainali ya Kombe la Muungano inatarajia kuchezwa Jumatano Aprili 29, 2026 kwenye uwanja huo huo wa New Amaan kuanzia saa mbili usiku.
Kimataifa Yanga yaipiga Azam, yafuzu fainali Muungano
Yanga yaipiga Azam, yafuzu fainali Muungano
Read also
