Madrid, Hispania
Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone amesema kwa sasa hamfikirii hata kidogo mpinzani wake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, timu ya Arsenal badala yake anawaza atakavyoikabli Athletic Club katika Ligi Kuu Hispania au La Liga.
Atlético Madrid imekuwa ikiandamwa na matokeo mabaya katika mechi zake za karibuni, imetoka kupoteza mechi nne za mwisho za Ligi Kuu Hispania huku ikisubiri kuingia katika mtihani mzito dhidi ya Arsenal.
Arsenal itakuwa mgeni wa Atletico Madrid Jumatano, Aprili 29, 2026 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa Atletico mechi hiyo ni mtihani wa pili kwani ina kazi ya kusaka nafasi nne za juu katika La Liga ili ipate tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao hivyo mechi yao ya Jumamosi Aprili 25, 2026 dhidi ya Athletic Club pia ina umuhimu wa kipekee.
Atletico inashika nafasi ya nne ikiwa imeizidi pointi nane Real Betis iliyo nafasi ya tano zikiwa zimebaki mechi sita kabla ya ligi hiyo kubwa nchini Hispania kuhitimishwa.
Kiwango cha Atletico hata hivyo kinatia hofu kwamba lolote linaweza kutokea na huenda msimu ujao timu hiyo ikakosa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kama haitokaza mkanda.
Kiujumla timu hiyo imepoteza mechi saba kati ya nane huku ushindi pekee ambao wanajivunia ni ule wa mabao 2-0 dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Alipoulizwa kuhusu ni kwa kiwango gani anaifikiria Arsenal, Simeone hata hivyo alisema hakuna anachofikiria badala yake ana utaratibu wa kuzipa umuhimu ule ule mechi zote.
“Hakuna ninachofikiria, tuna umuhimu ule ule tunaojaribu kuuweka katika mechi zote, tutajaribu kuuweka mchezo tunapoona tunaweza kuwaumiza,” alisema Simeone.
