Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema anafurahia kuiangalia timu ya Arsenal ikicheza kwa kuwa anajifunza mambo mengi kupitia timu hiyo kwa namna tofauti.
Aresenal au Gunners wako mstari wa mbele katika mbio za kusaka mataji mawili ya Ligi Kuu England pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Katika ligi kuu timu hiyo inashika usukani kwa tofauti ya pointi sita na katika Ligi ya Mabingwa wanasubiri kuumana na Atletico Madrid katika hatua ya nusu fainali.
Pamoja na mafanikio hayo, staili ya uchezaji wa timu hiyo chini ya kocha Mikel Arteta imeendelea kupingwa kila kona kwa kinachotajwa kuwa asilimia 37 ya mabao yao 62 ya kwenye ligi yamefungwa kwa ‘set pieces’.
Arsenal chini ya Arteta ambaye amewahi kufanya kazi na Pep,, Jumapili Aprili 19, 2026 itasafiri hadi Manchester kuumana na Man City, timu ambayo inashika nafasi ya pili kwenye ligi hivyo ushindi ndio kitu pekee wanachohitaji Arsenal.
Ushindi utaiweka Arsenal katika mazingira mazuri ya kubeba taji la ligi hiyo msimu huu wa 2025-26 baada ya kulikosa kwa takriban miaka 22 sasa.
Kwa upande wake Pep alipoulizwa kama anafurahia kuwaona Arsenal wakicheza alijibu ndio na kufafanua kwamba anajifunza mambo mengi katika namna tofauti na anafahamu kwamba timu hiyo ina kitu cha kipekee.
“Watu wanachotaka ni kushinda na tutapambana, jambo la msingi hasa ni kwamba hatutapambana dhidi ya Arsenal iliyokosa taji kwa miaka 22, wana kitu kinachowafanya wawe wa kipekee, hilo ninalifahamu,” alisema Pep.
Pep alisisitiza kwamba wana wajibu wa kuwa makini na aina yao ya uchezaji na hicho ndicho kitu pekee wanachotakiwa kukipigania badala ya kupambana na rekodi ya Arsenal ya miaka 22 bila taji.
