Florida, Marekani
Mwanasoka nyota wa Argentina Lionel Messi amepewa heshima ya kipekee na klabu yake ya Inter Miami ambayo imeamua jukwaa moja katika uwanja wao mpya litaitwa kwa jina la mchezaji huyo yaani Lionel Messi Stand.
Messi, 38, mmoja wa wanasoka mahiri duniani alijiunga na Inter Miami ya Marekani mwaka 2023 na kuanza kucheza katika ligi kuu nchini humo maarufu MLS baada ya kujipatia mafanikio barani Ulaya na klabu za Barcelona na PSG.
Akiwa na Inter Miami, Messi amefanikiwa kuweka rekodi ya mabao 82 na asisti 53, moja ya mafanikio ambayo yameifanya klabu hiyo kumpa heshima ya jina lake kutumiwa katika moja ya majukwaa ya uwanja wao mpya.
Taarifa ya Intert Miami ilieleza kuwa kwa utamaduni uliozoeleka heshima za aina hiyo hutolewa kwa kuangalia mambo yaliyopita na ya kihistoria lakini kwa hili ni tofauti, limetokana na mambo mazuri ya wakati huu.
“Heshima hii ni kwa mambo yanayoendelea wakati huu, ni kwa kinachoonekana wakati wote Messi akiwa uwanjani, kumpa mtu heshima si kila wakati huwa ni kufunga ukurasa, kuna wakati ni kutambua kwamba unashuhudia kitu cha kipekee,” ilieleza taarifa ya Inter Miami.
Inter Miami wanatarajia kucheza mechi yao ya kwanza katika uwanja wao mpya dhidi ya Austin FC, mechi ambayo imepangwa kuchezwa Aprili 4, 2026.
Hii ni mara ya pili kwa Messi kupewa heshima ya aina hiyo, awali ilikuwa katika klabu yake ya utotoni ya Newell’s Old Boys ya kwao Argentina ambayo Juni, 2025 ilitangaza kutumia jina la mchezaji huyo katika moja ya majukwaa yake.
Kujiunga kwa Messi katika klabu ya Inter Miami ambayo mmoja wa wamiliki wake ni nahodha wa zamani wa England, David Beckham pia kumesaidia kulitangaza na kulipa umaarufu soka la Marekani na ligi ya MLS.
