Paris, Ufaransa
Mwanasoka mkongwe wa Ufaransa, Zinedine Zidane ‘Zizou inadaiwa amekubali kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa na ataanza rasmi kazi hiyo baada ya fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazoanza kutimua vumbi Juni 11 mwaka huu.
Chanzo kimoja cha habari kimeeleza kuwa Zizou, 53, amefanya mazungumzo ya awali na mabosi wa Shirikisho la Soka Ufaransa (FFF) na kukubali kuchukua nafasi ya kocha wa sasa wa timu hiyo, Didier Deschamps.
Zizou alianza kazi ya ukocha mwaka 2012 na kujipatia mafanikio akiwa na Real Madrid, timu ambayo aliinoa kwa vipindi viwili kati ya mwaka 2016 hadi 2018 na 2019 hadi 2021 na kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na timu ya taifa ya Ufaransa.
Katika enzi zake za soka la ushindani, Zizou alikuwa mmoja wa viungo mahiri aliyewahi kutwaa tuzo ya Ballon d’Or mwaka 1998 na kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 1998, 2000 na 2003.
Akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa mbali na kuiwezesha timu hiyo kubeba taji la dunia mwaka 1998, Zizou anakumbukwa kwa kumpiga kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2006, mechi ambayo Italia ilishinda na kubeba taji la dunia.
Akiwa kocha Real Madrid, Zizou aliiwezesha timu hiyo kubeba mataji ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kuachana nayo mwaka 2021 na tangu wakati huo amekuwa bila timu.
Zizou na Deschamps walikuwa pamoja katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kulichobeba ubingwa wa dunia mwaka 1998 nchini Ufaransa baada ya kuibwaga Brazil katika mechi ya fainali.
Kimataifa Zizou kumrithi Deschamps Ufaransa
Zizou kumrithi Deschamps Ufaransa
Read also
