Na mwandishi wetu
Simba imechupa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kuinyuka TRA United mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa Jumapili Machi 22, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo Simba imefikisha pointi 31 ikiizidi Azam FC iliyokuwa nafasi ya pili na pointi 29 ingawa Simba imecheza mechi 14 na Azam 15 wakati vinara wa ligi hiyo Yanga wana pointi 38 baada ya kuingia dimbani mara 16.
Ukurasa wa mabao ya Simba ulifunguliwa dakika ya 25 kwa bao la mkwaju wa penalti iliyopigwa na Seleman Mwalimu, penalti ambayo ilitolewa baada ya Nickson Kibabage kuchezewa rafu ndani ya eneo la penalti.
Simba waliendelea kuutawala mchezo wakifanya mashambulizi ya kusaka bao la pili huku TRA wakionesha uhai katika ulinzi na kufanya mashambulizi machache lakini hadi dakika 45 zinakamilika matokeo yalibaki 1-0.
Kasi ya mashambuzi ya Simba iliendelea na hatimaye kuzaa matunda katika dakika ya 67 kwa bao la mpira wa adhabu lililopigwa kwa umahiri na Neo Maema na kuwapita wachezaji wa TRA waliojipanga kuzuia.
Simba walikamilisha hesabu zao dakika moja kabla ya kutimia dakika 90 kwa bao la Yusuph Kagoma aliyeujaza mpira wavuni kwa kichwa baada ya kuiwahi krosi.
Soka Simba yairarua TRA 3-0
Simba yairarua TRA 3-0
Related posts
Read also
