Tehran, Iran
Shirikisho la Soka Iran limesisitiza kuwa nchi yao inaipinga Marekani na si fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini humo kuanzia Juni 11, 2026.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari nchini Iran, Far News Agency, chanzo hicho kimemnukuu kiongozi mkuu wa Shirikisho la Soka Iran, Mehdi Taj akitoa msimamo huo Jumatano Machi 18, 2026.
Katika siku za hivi karibuni msimamo wa Iran kushiriki fainali hizo ambazo Marekani itakuwa mwenyeji na nchi za Mexico na Canada, umekuwa njia panda tangu Marekani na Israel zifanye mashambulizi ya anga nchini Irani mwishoni mwa mwezi uliopita.
Timu ya taifa ya Iran katika fainali hizo inatarajia kucheza mechi zake tatu za awali nchini Marekani na kwa mujibu wa Taj, watajiandaa kwa mechi hizo lakini wataipinga Marekani na si fainali za Kombe la Dunia.
Taj pia alitumia mtandao wa Twitter au X kufafanua kuwa katika mkakati huo wa kuipinga Marekani, kwa sasa wapo katika mazungumzo na Fifa kwa lengo la kuhakikisha mechi zao zinahamishiwa nchini Mexico.
“Rais Donald Trump aliposema wazi kwamba hawezi kuihakikishia usalama timu ya taifa ya Iran, maana yake ni kwamba hatuwezi kwenda Marekani, tunawasiliana na Fifa ili mechi zetu zihamishiwe Mexico,” alisema Taj.
Kwa upande mwingine Rais wa Fifa, Gianni Infantino alinukuliwa akisema kwamba anatarajia timu zote zilizofuzu fainali za Kombe la Dunia kushiriki katika misingi ya haki na kuheshimiana na matumaini ya Fifa ni kuona fainali hizo zinafanyika kama zilivyopangwa.
Ikitokea mechi za Iran kuhamishiwa Mexico bado timu hizo zinaweza kukutana katika raundi ya pili ya michuano hiyo nchini Marekani kwa kuzingatia nafasi zitakazoshika katika makundi yao.
