Na mwandishi wetu
Matokeo ya sare ya 0-0 yameendelea kushika kasi kwa timu ya Yanga katika Ligi Kuu NBC baada ya kupata matokeo hayo mara nyingine katika mechi na TRA United iliyopigwa Jumatano Machi 18, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Hii ni sare ya tatu katika mechi za hivi karibuni za timu hiyo baada ya kupata matokeo kama hayo dhidi ya Simba na Azam FC na sasa TRA United.
Yanga hata hivyo ilicheza mechi hiyo bila ya wachezaji wake kadhaa tegemeo kina Dickson Job, Ibrahim Bacca, Depu na wengineo na kama hiyo haitoshi timu hiyo ilipata pigo baada ya mshambuliaji wake Prince Dube kushindwa kumaliza mchezo.
Dube aliyeianza mechi kwa matumaini makubwa aliishia dakika ya 21 na nafasi yake kuingia Emmanuel Mwanengo ambaye dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili alipata nafasi ya kufunga lakini mpira wa kichwa alioupiga uliokolewa.
Safu ya ulinzi ya Yanga pamoja na kuwakosa nyota wake mahiri lakini ikiwa chini ya kipa Djigui Diarra, Bakari Mwamnyeto na Frank Assinki ilifanikiwa kudhibiti mashambulizi ya hapa na pale ya TRA.
TRA kwa muda mrefu ilipambana ikitengeneza mashambulizi kutokea pembeni yakiongozwa na Ramadhan Chobwedo na Joseph Akandwabo lakini uimara wa mabeki wa pembeni wa Yanga, Mohamed Hussein aliyekuwa upande wa kushoto na Israel Mwenda aliyekuwa kulia walidhibiti mashambulizi hayo.
Mwenda naye hakuweza kumaliza dakika zote 90 kwani mapema kipindi cha pili alitolewa na nafasi yake kuingia Yao Kouassi ambaye amekuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Mambo yaliwaendea kombo TRA na kulazimika kucheza na wachezaji 10 kwa takriban dakika 20 baada ya Mzamiru Yassin kupewa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje ingawa TRA walijipanga vizuri kwa dakika zilizobaki na kuidhibiti Yanga.
Mara baada ya dakika 90 kukamilika, Yanga walionekana kuwa katika hali ya huzuni wakati kwa TRA ilikuwa shangwe wakifurahia matokeo ya sare dhidi ya Yanga ambao pia ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo.
Sare hiyo hata hivyo haijaweza kuishusha Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, badala yake timu hiyo inaendelea kushika usukani ikiwa na pointi 37 katika michezo 15 ikijivunia kutopoteza mchezo hata mmoja.
Kimataifa Matokeo ya sare yaongezeka Yanga
Matokeo ya sare yaongezeka Yanga
Read also
