Cairo, Misri
Bodi ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeivua timu ya taifa ya Senegal taji la Afcon 2025 kwa kosa la kwenda kinyume na kanuni namba 84 na kuifutia ushindi wa bao 1-0 badala yake imeipa Morocco ushindi wa ‘mezani’ wa mabao 3-0.
Senegal imevuliwa taji hilo kwa kosa la kugomea mechi kwa takriban dakika 17, tukio lililotokea katika mechi ya fainali baina ya timu hizo iliyopigwa Januari 18 na timu hiyo kugomea mechi kwa madai kwamba mwamuzi alikuwa akiwabeba wenyeji Morocco.
Uamuzi huo wa CAF umetokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Shirikisho la Soka la Morocco ambapo Bodi ya Rufaa ya CAF iliona kuna kosa kwa upande wa Shirikisho la Soka Senegal kupitia timu yao ya taifa.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa mjini Rabat, Senegal walisusia penalti iliyotolewa baada ya El Hadji Malick Diouf kumuangusha Brahim Diaz katika eneo la penalti ingawa Diaz aliyepewa kupiga penalti hiyo alikosa.
Senegal au Simba wa Teranga walizitumia vyema dakika 30 za nyongeza kupata bao pekee na la ushindi dakika ya tatu (93) kwa mpira ulioanzia kwa pasi ya kisigino ya Mane aliyemuunganishia Idrissa Gana Gueye naye kumpasia Pape Gueye aliyeujaza wavuni.
Uamuzi wa CAF kuivua Senegal taji ambalo walilipigania kwa mbinde baada ya mechi iliyochezwa kwa dakika 120, umezua taharuki miongoni mwa wadau wa soka duniani kote.
Mmoja wa watu waliojitokeza hadharani kupinga uamuzi huo ni kiungo wa zamani wa Arsenal, Man City na timu ya taifa ya Ufaransa, Samir Nassir ambaye alionesha kushtushwa na uamuzi huo akisema si sahihi.
Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Senegal, Abdoulaye Seydou amehoji uhalali wa uamuzi huo ambao wanaona ni kama vile hautokani na taratibu za kisheria badala yake kulikuwa na maelekezo.
Shirikisho hilo linadaiwa kuanza mchakato wa kupinga uamuzi huo kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) wakati baadhi ya wachezaji wa Senegal wakidai kwamba hawatorudisha medali za ushindi huo huku Idrissa Gueye akisisitiza kwamba mafanikio yao ya kihistoria katika mji wa Rabat hawawezi kuacha yapotee.
Serikali ya Senegal nayo imeingilia kati suala hilo ikisema kwamba uamuzi huo umetokana na makosa ya kutafsiri sheria na hivyo kuja na uamuzi ambao si wa haki.
Kimataifa CAF yaivua Senegal taji la Afcon
CAF yaivua Senegal taji la Afcon
Read also
